CCM YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA ASKOFU MKUU RUWA’ICHI KUFUATIA KIFO CHA KADINALI PENGO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, February 26, 2026

CCM YATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA ASKOFU MKUU RUWA’ICHI KUFUATIA KIFO CHA KADINALI PENGO


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa salamu za rambirambi kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa’ichi OFMCap, kufuatia kifo cha Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo hilo, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo, aliyefariki dunia Februari 19, 2026, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alipokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza Februari 26, 2026 baada ya kusaini kitabu cha maombolezo katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam, Katibu Mkuu CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro, alisema amewasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Migiro alisema marehemu Kadinali Pengo atakumbukwa kama mchungaji wa faraja na tumaini, kiongozi wa kiroho mwenye hekima, unyenyekevu na msimamo thabiti wa maadili.

Alijipambanua si tu kwa huduma ya Kanisa, bali pia kwa mchango wake katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa, maadili ya jamii, malezi ya vijana na uwajibikaji wa viongozi.

“Kadinali Pengo ameacha alama inayodumu ya utumishi wa Mungu, utumishi wa Taifa na utumishi wa jamii. Maisha na mafundisho yake yataendelea kuwa dira kwa vizazi vijavyo,” alisema Dkt. Migiro.

CCM imesema inaliombea Kanisa Katoliki na waumini wote wapate faraja katika kipindi hiki cha maombolezo na Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.

Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi, mwili wa marehemu utawasili Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Februari 27, 2026 kwa ajili ya waumini kutoa heshima zao za mwisho, na Ibada ya Misa ya Mazishi itafanyika Februari 28, 2026 katika Kituo cha Hija Pugu, Dar es Salaam.



No comments:

Post a Comment