
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, amefanya kikao na uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) leo tarehe 19 Februari 2026 jijini Dodoma.
Kikao hicho kililenga kujadili namna ambavyo Wizara ya Nishati na NBC wanavyoweza kushirikiana katika kuwawezesha wawekezaji wazawa, hususan katika sekta ya mafuta na gesi.
Dkt. Mataragio ameipongeza NBC kwa utayari wake wa kuwainua wawekezaji wazawa, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi, hasa kupitia sekta ya nishati. Ameeleza kuwa wapo wadau wengi wazawa wenye nia ya kuwekeza katika mafuta na gesi, lakini wanakumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa mitaji wezeshi ya kutekeleza miradi hiyo.
“Ujio na ushirikiano wenu utasaidia kuwainua wawekezaji wazawa ili waweze kumudu na kuwekeza kikamilifu hapa nchini,” amesisitiza Dkt. Mataragio.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inatamani kuona wawekezaji wazawa wanajenga viwanda, kuanzisha biashara, na kuajiri vijana ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira nchini. Pia alibainisha kuwa sekta ya nishati inapaswa kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa taifa, huku wawekezaji wazawa wakichukua nafasi muhimu katika maendeleo ya sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NBC anayeshughulikia wateja wakubwa na Serikali, Bw. Elvis Ndunguru, amesema benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo kwa wawekezaji wadogo na wakubwa ili kusaidia kukuza biashara zao.
Benki ya Taifa ya Biashara imekuwa ikishirikiana na Serikali na taasisi mbalimbali kutoa huduma za kifedha kwa wawekezaji, hasa katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji. Sisi kama NBC tupo tayari kushirikiana na Wizara ili kufikia malengo ya Serikali ya kuwawezesha wawekezaji, hususan wazawa,” amesema Ndunguru.
Wizara ya Nishati na NBC zimekubaliana kufanya kazi kwa pamoja ili kuwainua wawekezaji wazawa katika sekta ya nishati kwa lengo la kukuza uwekezaji wa ndani, kutengeneza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi nchini.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya sekta ya nishati nchini na kusaidia utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.



No comments:
Post a Comment