Na.Mwandishi Wetu
Taasisi ya Jafo Education Foundation imefadhili jumla ya vijana 51 kusoma katika Chuo cha FDC Kisarawe - Mzenga, kwa lengo la kuwawezesha kupata ujuzi wa fani mbalimbali za ufundi.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi na kuzungumza na wananchi katika Kata ya Mzenga, Mbunge wa Jimbo la Kisarawe Mhe.Dkt. Selemani Jafo, amesema vijana hao 51 watatoka katika kata zote 17 za wilaya hiyo na taasisi hiyo itagharamia ada zao za masomo.
"Hii ni fursa muhimu kwa vijana wa Kisarawe kujipatia ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa, hasa katika kipindi hiki ambacho soko la ajira linahitaji wataalamu wenye ujuzi wa vitendo."amesema Dkt. Jafo
Dkt.Jafo amesema kuwa Chuo cha FDC Kisarawe – Mzenga ni chuo kipya kilichojengwa wilayani humo na tayari kinatoa mafunzo katika fani mbalimbali zikiwemo ufundi magari, ushonaji, ujenzi, mapishi, umeme, kompyuta pamoja na mafunzo ya muda mfupi.
Aidha, Dkt. Jafo ameeleza kuwa tangu mwaka 2010 amefanikiwa kusaidia zaidi ya vijana 500 kutoka familia zenye changamoto kusoma katika ngazi mbalimbali, ikiwemo kidato cha tano, astashahada, stashahada na shahada.
Katika kuendeleza juhudi za kukuza elimu ya ufundi, tarehe 20 Februari, Dkt. Jafo kupitia taasisi yake amekabidhi msaada wa vyerehani vinne vya umeme katika chuo hicho, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa dhamira kuu ni kuwawezesha vijana katika fani za ufundi ili kujenga msingi imara wa ajira rasmi na zisizo rasmi, pamoja na kuongeza kasi ya maendeleo katika Wilaya ya Kisarawe.




No comments:
Post a Comment