Na Mwandishi Wetu - Mtwara
Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Serikali imewekeza zaidi ya sh. trilioni moja katika utekelezaji wa miradi ya gesi asilia mkoani Mtwara ili kuongeza uzalishaji, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia.
Akizungumza katika ziara yake ya kukagua miradi hiyo, Waziri Ndejembi amesema utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima vya gesi Ntorya pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Ntorya hadi Madimba, na uchorongaji wa visima katika Kitalu cha Mnazi Bay utaongeza kiasi kikubwa cha gesi kwa ajili ya uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwandani na majumbani.
Amesema mahitaji ya gesi asilia nchini yanaongezeka kwa kasi, hivyo Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha sekta hiyo ili kukidhi mahitaji ya wateja wanaozidi kuongezeka.
“Miradi hii uwekezaji wake ni mkubwa Serikali imetoa kipaumbele katika eneo la Gesi asilia na sote tunajua mahitaji ya gesi asilia yanakua kwa kasi sana nchini. Wateja wamekuwa wengi hivyo changamoto hii muichukue kama fursa kwa kushirikiana na wabia wenu na Wakandarasi, muitekeleze miradi hii itakayoongeza gesi asilia, kwa kasi na ufanisi mkubwa,"amesisitiza.
Waziri Ndejembi ameelekeza kuanzia Septemba 2026 uzalishaji wa gesi katika eneo la Ntorya uanze rasmi ili kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika na kuchochea shughuli za kiuchumi hususan katika Ukanda wa Kusini na maeneo mengine ya nchi.
Amebainisha kuwa jitihada hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kutoa fedha na miongozo madhubuti ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Aidha, Waziri Ndejembi amesisitiza umuhimu wa kuendelea na utafiti pamoja na uchimbaji wa visima vipya ili kuongeza uzalishaji na kuhakikisha nchi inanufaika kikamilifu na rasilimali zake za ndani.
Pia amelielekeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhakikisha linarejesha kwa jamii kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika maeneo yanayozunguka miradi ya gesi, ili wananchi wanufaike moja kwa moja na uwekezaji huo kwa kushirikiana na halmashauri husika.












No comments:
Post a Comment