PPAA YAOKOA SHILINGI BILIONI 586.5, YAZUIA ZABUNI 43 ZISIZOKIDHI VIGEZO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, February 25, 2026

PPAA YAOKOA SHILINGI BILIONI 586.5, YAZUIA ZABUNI 43 ZISIZOKIDHI VIGEZO



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, Dodoma


Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeokoa Shilingi bilioni 586.5 baada ya kuzuia utoaji wa zabuni 43 zilizokuwa zimetolewa kwa wazabuni waliokosa uwezo wa kifedha na sifa za kitaalamu za kutekeleza miradi husika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando, alisema hatua hiyo imezuia utekelezaji usioridhisha wa miradi ambao ungesababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.

Amesema kupitia kitengo cha rufaa, Mamlaka imesajili mashauri 196 yaliyotokana na michakato mbalimbali ya ununuzi wa umma. Kati ya mashauri hayo, zabuni 43 zenye thamani ya Shilingi bilioni 586.5 zimezuiwa kutolewa kutokana na wazabuni husika kutokidhi vigezo vya kifedha na kitaalamu.

“Hatua hii imelenga kulinda maslahi ya umma na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika,” alisema Sando.

Katika hatua nyingine, Sando alisema katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika sekta ya ununuzi wa umma, Mamlaka imekamilisha moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST).

Amefafanua kuwa moduli hiyo imerahisisha usajili na ushughulikiaji wa malalamiko na rufaa, na kuongeza uwazi katika mchakato wa ununuzi wa umma. Tangu kuanza kutumika kwake, jumla ya malalamiko 549 yamewasilishwa na kushughulikiwa na taasisi nunuzi, huku rufaa 26 zikiwasilishwa na kuamuliwa na Mamlaka ya Rufani kupitia mfumo huo.

Kwa mujibu wa Sando, matumizi ya moduli hiyo yameongeza ufanisi, kupunguza muda wa kushughulikia mashauri na kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa haki.

Aidha, amesema katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuwawezesha vijana na makundi maalum, PPAA imetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana 878 katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ili waweze kushiriki kikamilifu na kudai haki zao katika michakato ya ununuzi wa umma.

Amewahimiza wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma kushiriki mafunzo hayo yanapotangazwa ili kuongeza uelewa wa matumizi sahihi ya moduli hiyo na taratibu za rufaa.





No comments:

Post a Comment