SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA CHUO CHA USTAWI WA JAMII, KUTOA WATAALAMU BORA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, February 23, 2026

SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA CHUO CHA USTAWI WA JAMII, KUTOA WATAALAMU BORA




Na Jackline Minja WMJJWM-Dar Es Salaam


Serikali itaendelea kukiimarisha Chuo cha Ustawi wa Jamii ili kiendelee kuzalisha wataalamu wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za kijamii na kuchangia maendeleo ya taifa, sambamba na kuboresha miundombinu na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Chuo hicho mkoani Dar Es Salaam, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema, Serikali inatambua nafasi ya Chuo hicho katika kuandaa wataalamu wa ustawi wa jamii watakaosaidia kuimarisha huduma za kijamii nchini ambapo Serikali itaendelea kushirikiana na uongozi wa Chuo hicho pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha changamoto za miundombinu ikiwemo upungufu wa hosteli na kumbi za mihadhara zinapatiwa ufumbuzi ili kuboresha zaidi mazingira ya kujifunza.

“Serikali inatambua kuwa uwekezaji katika miundombinu ya Chuo cha Ustawi wa Jamii ni uwekezaji katika ustawi wa taifa, hatuwezi kuzungumzia maendeleo jumuishi bila kuwa na taasisi imara zinazozalisha wataalamu wa kusimamia ustawi wa jamii, afya ya akili, malezi, ujumuishi na haki za makundi maalum pia Serikali itaweka suala la ujenzi wa miundombinu ya Chuo katika vipaumbele vyake na kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo pamoja na sekta binafsi ili kuhakikisha miradi ya ujenzi inatekelezwa kwa wakati na kuongeza ubora wa mazingira ya kujifunzia” amesema Mahundi.

Awali akisoma taarifa ya Chuo, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Joyce Nyoni amesema, Chuo hicho kimeendelea kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa ushauri elekezi unaochangia kuboresha ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi ambapo katika mwaka wa masomo 2025/2026, chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 5,868 ambapo wanawake ni 3,823 na wanaume 2,045, hali inayoonesha ongezeko la udahili na uhitaji mkubwa wa wataalamu wa ustawi wa jamii nchini.

“Katika kutekeleza majukumu yake, taasisi imekuwa ikizingatia sera na mikakati ya kitaifa na kimataifa ya kiuchumi, ustawi na maendeleo ya jamii kama vile Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Ilani ya Chama cha Mapinduzi za nyakati mbalimbali na Malengo Endelevu ya Maendeleo taasisi inaendelea kubadilisha maisha ya mtu mmoja mmoja na jamii kwa kutoa mafunzo bora, kufanya tafiti na kutoa ushauri elekezi unaolenga kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Taifa, hatua inayosaidia kujenga jamii yenye ustawi na maendeleo endelevu” amesema Dkt. Nyoni.

Ziara hiyo imelenga kujionea utekelezaji wa majukumu ya Chuo hicho pamoja na kujadili mikakati ya kukiimarisha ili kiendelee kuwa kitovu muhimu cha kuzalisha wataalamu wa ustawi wa jamii watakaosaidia kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.


No comments:

Post a Comment