Na Veronica Mwafisi-Tanga
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuinua elimu na kukuza uchumi wa wananchi katika Mkoa wa Tanga kupitia mradi wa ujenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Kampasi ya Tanga ambao umeanza kutekelezwa katika Kata ya Maweni, Kange tarehe 8 Februari, 2025.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 20 Februari, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete alipokuwa akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma na wananchi wa Mkoa wa Tanga mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo na kabla ya kuweka jiwe la msingi.
Waziri Kikwete amesema Kampasi hiyo ikikamilika inategemea kuchukua jumla ya wanafunzi 2,000 lakini watakaonufaika sio wanafunzi hao pekee ambao watapata elimu, bali na wananchi ambao watafanya shughuli mbalimbali za maendeleo na kuweza kuinua kipato chao.
Amemshukuru Mhe. Rais kwa kutambua umuhimu wa elimu katika mkoa huo na kutoa maelekezo ya kujenga kampasi hiyo.
Aidha, Mhe. Kikwete amewashukuru na kuwapongeza wananchi wa Mkoa wa Tanga Kange kwa uzalendo wao mkubwa wa kutoa eneo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo eneo hilo linapojengwa chuo hicho ili watoto wao wapate elimu.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha mambo yote yenye athari chanya yanatekelezwa kwa ufanisi wa hali ya juu.
Ameupongeza uongozi na Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma kwa usimamizi mzuri wa ujenzi. “Mimi sio mtaalam wa ujenzi lakini kwa macho unaona kazi iliyofanyika ni nzuri na inaridhisha, hongereni sana, Mhe. Kikwete ameongeza.
Ametoa wito kwa watendaji wa Kampasi hiyo kuweka mazingira mazuri ya eneo hilo kwa kupanda miti ya matunda na kivuli.
Amewasistiza wananchi kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kulinda miundombinu ya Kampasi hiyo na ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu-UTUMISHI, SACP Ibrahimu Mahumi amemshukuru Mhe. Kikwete kwa maelekezo yake ya kuboresha utendaji kazi ambayo amekuwa akiyatoa mara kwa mara kwa taasisi zilizo chini ya ofisi anayoisimamia.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba ameishukuru Serikali kwa uamuzi walioufanya wa kujenga Chuo hicho kwani wangeweza kujenga popote.
Mhe. Waziri kazi hii nzuri inayoonekana ni maelekezo yako ambayo umekuwa ukiyatoa mara kwa mara kwa watendaji katika taasisi zilizo chini ya Ofisi yako, ameongeza,
Mhe. Kolimba ameahidi yeye pamoja na viongozi wengine wa mkoa kusimamia kwa umakini ujenzi wa chuo hicho na kukamilika kwa wakati ili kianze kutumika kama ilivyotarajiwa.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Kampasi hiyo, Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho amemshukuru Mhe. Kikwete kwa kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi na kuweka jiwe la msingi.
Dkt. Mabonesho amesema kukamilika kwa Kampasi hiyo kutasaidia kuokoa fedha nyingi za pango ambazo wamekuwa wakilipa sasa.









No comments:
Post a Comment