TANESCO YAENDELEA KUPOKEA MAGARI KUBORESHA HUDUMA KWA WATEJA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, February 26, 2026

TANESCO YAENDELEA KUPOKEA MAGARI KUBORESHA HUDUMA KWA WATEJA


Katika jitihada za kuendelea kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wateja wake, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepokea magari mapya 12 katika awamu ya pili kati ya magari 205 yanayotarajiwa kuwasili ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili.

Hatua hii ambayo ni sehemu ya mkakati wa muda mfupi uliotekelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw. Lazaro Twange inalenga kuongeza kasi na ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yamebainishwa Februari 21, 2026 na Meneja wa Huduma za Usalama wa TANESCO, Bw. Lenin Kiobya, wakati akizungumza katika zoezi la kupokea magari hayo lililofanyika katika Ofisi za TANESCO, Ubungo, Jijini Dar es Salaam.

Bw. Kiobya amesema kwamba magari hayo yatakuwa na mchango mkubwa katika kuwafikishia wananchi huduma ya umeme kwa wakati, hususan katika maeneo yenye changamoto za kimazingira na ambayo awali hayakuwa rahisi kufikika.

“Magari haya yatasaidia sana kufanikisha malengo makubwa ya shirika, ikiwemo mpango wa Mission 300 unaolenga kuongeza idadi ya wananchi wanaotumia umeme nchini. Tunawaomba madereva watakao kabidhiwa magari haya kuyatunza vyema ili yaendelee kusaidia kikamilifu katika shughuli za kila siku,” alisema Bw. Kiobya.

Kwa upande wake, Bw. Thomas Gowele, Msimamizi wa Kitengo cha Usafiri TANESCO, amesema kwamba magari hayo ni ya kisasa yakiwa na mfumo wa kamera mbele na nyuma ili kurahisisha dereva kuona vizuri wakati wa majukumu yake. Aidha, magari hayo yameambatanishwa na mashine ya kuinua mizigo (crane) yenye uwezo wa kuzunguka nyuzi 360°, ambayo itarahisisha kupandisha na kushusha nguzo pamoja na vifaa vingine.

“Magari haya ni ya kisasa, yamebuniwa kuboresha utoaji wa huduma zetu huku yakiweka kipaumbele cha usalama wa wafanyakazi,” alisema Bw. Gowele.

TANESCO inaendelea kuwekeza katika ununuzi wa vitendea kazi vya usafiri, ikiwa ni pamoja na magari madogo, malori, bajaji na pikipiki, ili kuhakikisha maeneo yote yanayohitaji huduma ya umeme yanafikiwa kwa urahisi na ufanisi zaidi.

No comments:

Post a Comment