
Jeshi la Polisi Tanzania Mkoa wa Dodoma limeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa kuwajengea uwezo watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na Polisi Kata.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Afisa Mnadhimu wa Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Willium Mwamamfupa Februari 24, 2026, ambapo amewataka watendaji hao kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha vitendo vya uhalifu vinazuiwa na kufikia ukomo.
ACP Mwamamfupa amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii ili kujenga uelewa, kuhamasisha chuki dhidi ya uhalifu na kuhimiza utoaji wa taarifa mapema kwa vyombo husika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma, ASP Crister Kayombo, ameeleza mikakati ya dawati hilo katika kuwahudumia wananchi kwa weledi na wepesi, akisisitiza hatua madhubuti dhidi ya wahalifu ikiwemo kuwakamata, kufanya upelelezi wa kina na kuwafikisha mahakamani.





No comments:
Post a Comment