‎WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA MKAKATI WA KITAIFA WA KISEKTA WA KUTOKOMEZA UKEKETAJI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, February 13, 2026

‎WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA MKAKATI WA KITAIFA WA KISEKTA WA KUTOKOMEZA UKEKETAJI



Na Saidi Saidi WMJJWM – Arusha

‎Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua Mkakati wa Kitaifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji Nchini (2025/2026–2029/2030) katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji yaliyofanyika Februari 12, 2026, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha.

Uzinduzi wa mkakati huo unalenga kuimarisha juhudi za kitaifa za kulinda haki, afya na ustawi wa wanawake na watoto wa kike.

‎Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Gwajima amesema mkakati huo utaimarisha uratibu na ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo na jamii katika kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukeketaji. Ameeleza kuwa mikoa ya Arusha na Manyara ina viwango vya juu vya ukeketaji, hali inayohitaji hatua madhubuti na ushiriki wa kila mdau.

‎Dkt. Gwajima amesema kuwa katika kutokomeza ukeketaji ni muhimu sana kuwashirikisha wanaume kwa kuwapa elimu, kwani wao ndio wahamasishaji wakuu wa vitendo hivyo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Gwajima pia ameongoza maandamano ya wanaume kama ishara ya kuwataka kupinga ukeketaji. Aidha, amewashukuru wadau mbalimbali wanaoiunga mkono Serikali ikiwemo Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), C-SEMA, SOS Children’s Village, Compassion International Tanzania na mashirika mengine kwa mchango wao katika mapambano dhidi ya ukeketaji.

‎Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Gloriana Kimathi, amemshukuru na kumpongeza Waziri Dkt. Gwajima kwa kuichagua Wilaya ya Monduli kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo, akisema kuwa ujio wake na kufanyika kwa maadhimisho hayo umeamsha ari kubwa ya mapambano dhidi ya ukeketaji. Ameongeza kuwa Wilaya itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutokomeza ukeketaji.

‎Naye Katibu wa Viongozi wa Mila Wilaya ya Monduli (Laigwanan), Natuli Letema, amesema viongozi wa mila wataendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mkoa katika kutoa elimu ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na ukeketaji.

Ameeleza kuwa juhudi hizo zitazaa matunda kutokana na ari mpya iliyoamshwa na Waziri Dkt. Gwajima ya kuendelea kupambana na mila hatarishi, akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa jamii kubadilika na kulinda watoto wa kike.





No comments:

Post a Comment