WAZIRI MAVUNDE AZINDUA KIWANDA CHA KUZALISHA MKAA MBADALA MKOANI TABORA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, February 21, 2026

WAZIRI MAVUNDE AZINDUA KIWANDA CHA KUZALISHA MKAA MBADALA MKOANI TABORA


Na Mwandishi Wetu - Tabora


Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amezindua Kiwanda cha Rafiki Briquettes mkoani Tabora na kuielekeza Bodi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe katika Mgodi wake wa Kiwira.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupanua matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.


Akizungumza Februari 21, 2026 wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani 20 kwa siku, Waziri Mavunde, amesema kitasaidia kupunguza ukataji wa miti na kusaidia ukaushaji tumbaku mkoani Tabora. 

Ameongeza kuwa, uzinduzi huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuhusu matumizi ya nishati mbadala kwa ajili ya kukaushia tumbaku, na kuongeza kwamba, kiwanda hicho kilichogharimu shilingi bilioni 3 kitawanufaisha wakulima wanaozalisha wastani wa tani 95,000 kwa mwaka ambao awali walitegemea kuni.

Waziri Mavunde amesema kutokana na akiba kubwa ya makaa ya mawe Kiwira, kutachangia kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme.

 Amesisitiza kuwa matumizi ya nishati chafu yana athari kubwa kiafya na kimazingira, huku Serikali ikilenga kufikia zaidi ya asilimia 84 ya wananchi ifikapo mwaka 2034 kutumia nishati safi na salama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, amesema uzinduzi wa kiwanda hicho unaendeleza ajenda za kitaifa za kuongeza thamani madini na kuhamasisha nishati safi ya kupikia. Amesema Shirika tayari lina kiwanda cha ubia cha kusafisha dhahabu cha Mwanza Precious Metals Refinery na sasa linazalisha na kusambaza Rafiki Briquettes kutoka makaa ya mawe ya Kiwira.

Ameongeza kuwa ujenzi wa kiwanda kingine unaendelea Dodoma na vingine vitano vinatarajiwa kujengwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Geita, hatua itakayofikisha jumla ya viwanda sita nchini.

 Amesisitiza kuwa briquettes hizo zimethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na zitasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, huku kiwanda cha Tabora kikitarajiwa kutoa ajira 200 za moja kwa moja na zisizo rasmi.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Balozi Simon Sirro, ameainisha umuhimu wa usimamizi mzuri wa Serikali na Wizara husika katika kuendesha shirika kwa ufanisi. 

Amesisitiza kuwa briquettes zinazozalishwa na STAMICO ni bora na zina soko, na kutoa wito wa kuongeza uzalishaji.

Aidha, ameeleza kuwa ili shirika liweze kujiendeleza, ni lazima kushindana na kampuni nyingine za uchimbaji madini na kuanzisha kampuni tanzu zenye ufanisi. Amesema bodi ya STAMICO itaendelea kutekeleza maagizo ya Serikali, kuongeza mapato, na kutoa gawio kwa Serikali. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, ameipongeza Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) kwa kuunga mkono agenda ya nishati safi ya kupikia na mafanikio ya sekta ya madini. Amesema kutokana na mwenendo mzuri wa sekta hiyo, Kamati itaendelea kuunga mkono juhudi za Wizara.

Ameeleza kuwa Serikali imefanikiwa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kutoka asilimia 6 hadi 27, na kumpongeza Waziri akisema, “Lakini Mhe. Waziri, tumeona namna unavyohamasisha uwekezaji huko duniani na sasa hapa unahamasisha matumizi ya nishati safi.”

Tukio la uzinduzi wa kiwanda hicho, limekwenda sambamba na kugawa vyeti kwa mawakala na makontena kwa mawakala Rafiki Briquettes katika mikoa mitano ya Tabora, Kigoma, Katavi, Rukwa na Singida. Pia, shirika hilo limesaini Mkataba wa Makubaliano na Chama Kuu cha Ushirika wa Tumbaku Mkoa wa Tabora (WETCU) wa mashirikiano ya kuwaunganisha wakulima na STAMICO kutumia Rafiki Briquttes.

No comments:

Post a Comment