WAZIRI MKUU ANUSA WIZI MWINGINE MUHEZA - TANGA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, February 16, 2026

WAZIRI MKUU ANUSA WIZI MWINGINE MUHEZA - TANGA


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza wajumbe wa Kamati Mapokezi na Kamati za Ujenzi za mradi wa ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wakamatwe na kuhojiwa mara moja ili watoe taarifa juu ya upotevu wa vifaa vya mradi huo.

“Kuna nondo 700, Marine boards 500 na matofali 2,000... hivi vifaa havijulikani viko wapi. Wahusika kila siku mnaripoti kazini, na mishahara mnalipwa wakati ujenzi umesimama na hakuna hatua zinazochukuliwa,” amesema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt. Jumaa Mhina.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Februari 16, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Lusanga, kata ya Mgomeni, wilayani Muheza waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la ofisi hiyo itakayokuwa na ghorofa moja pindi ikikamilika.

“Kamanda wa TAKUKURU ninahitaji hii taarifa kwa kina kabla sijamaliza ziara yangu mkoani Tanga. OCD fuatilieni kwa kina ushiriki wa watumishi wa hii Halmashauri. Kila mmoja ahojiwe hadi tujue vifaa vilipoteaje.”

Amesema kuwa anazo taarifa kwamba timu ya manunuzi imenunua vifaa ambavyo vimewekwa stoo wakati hatua yake ya ujenzi haijafikiwa. “Nimeambiwa vifaa vingine vimekuja lakini vimekaa stoo tu. Ni kwa nini mmenunua wakati hamjamaliza hatua ya kwanza? Mshauri mwelekezi wa mradi yupo lakini hamsikilizi ushauri anaotoa,” alisema.

Jengo hilo ndiyo limemalizika kujengwa ghorofa ya chini, na linasubiri kuanza kuwekewa linta kwenye ghorofa ya kwanza.

Waziri Mkuu amekemea tabia ya kutochukua hatua masuala kama hayo yanapojitokeza hasa ikizingatiwa kwamba Halmashauri nyingine ambazo walipewa fedha kwa wakati mmoja wao wameshakamilisha kazi ya ujenzi.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Miundombinu na Maendeleo Mijini na Vijijini, Mhandisi Abdalla Jaha alisema mradi huo ambao umefikia asilimia 68, ulianza kujengwa Septemba 29, 2023 na wanatarajia ifikapo mwishoni mwa Juni, 2026 sakafu ya chini ianze kutumika.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa pongezi kwa kiwanda cha vifungashio cha Yogi PolyPack ambacho kiko Pongwe, nje kidogo ya Manispaa ya Tanga.

Akizungumza na viongozi na watumishi wa kiwanda hicho, Waziri Mkuu amesema uwekezaji uliofanywa ni mkubwa na kwamba serikali itaendelea kuhakikisha inatengeneza mazingira mazuri ya uzalishaji.

“Nimetembelea kiwanda, nimeona kazi nzuri ikiendelea na inatumia teknolojia ya kisasa. Haya ndiyo mambo Mheshimiwa Rais anataka kuyaona. Unatengeneza ajira, unazalisha bidhaa ambazo ni malighafi kwa viwanda vyetu hapa nchini na unatoa kipato kwa wafanyakazi wako,” amesema.

Mapema leo, Waziri Mkuu alitembelea bandari ya Tanga na kukagua shughuli za bandari hiyo na kisha kuzungumza na watumishi. 

Akiwa bandarini hapo, alipokea maelezo ya uboreshaji wa bandari hiyo kisha akatembelea eneo ambalo zitajengwa gati mbili mpya, katika bandari ya Tanga ikiwa ni mkakati wa Serikali ya kuiongezea uwezo bandari ya Tanga wa kutoa huduma shindani na za ufanisi.

Akizungumza na watumishi wa bandari ya Tanga, Waziri Mkuu aliahidi kwamba Serikali itahakikisha inaendelea kufanyia kazi changamoto zote za kiutumishi zinazowahusu watumishi hao.

“Serikali itaendelea kufanya maboresho katika bandari hii ili iweze kuhudumia idadi ya meli nyingi kwa kadiri inavyowezekana. Tunatambua ushindani wa kibiashara uliopo lakini tutaendelea kufanya maboresho ili tunufaike na nafasi ya kijiografia ya mkoa wetu,” alisema.

Pia ameiagiza Mamlaka ya Bandari ifanyia kazi changamoto ya uhaba wa vifaa vya kupakulia mizigo ili kuendana sambamba na maboresho hayo. 

No comments:

Post a Comment