WAZIRI MKUU Dkt.NCHEMBA ARIDHISHWA UJENZI DARAJA LA PANGANI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, February 15, 2026

WAZIRI MKUU Dkt.NCHEMBA ARIDHISHWA UJENZI DARAJA LA PANGANI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ameridhishwa na kasi ya ujenzi wadaraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 64.

Akizungumza alipokagua daraja hilo katika ziara yake inayoendelea mkoani Tanga Dkt. Nchemba ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha daraja hilo na barabara unganishi ujenzi wake unakamilika kwa wakati na ubora.

" Nawapongeza sana Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kazi nzuri mnayofanya, tembeeni kifua mbele, haya ni matunda ya uhuru", amesisitiza Dkt. Mwigulu.

"Hakikisheni barabara yote inakamilika kwa lami kuanzia Tanga-Pangani km 50 daraja la Pangani mita 525 , Mkange- Mkaja- Tungamaa km 95.2 na Bagamoyo-Makurunge km 64 ili kuufungua ushoroba wa pwani ya Afrika Mashariki upande wa Tanzania na hivyo kuchochea uchumi", amesisitiza Dkt. Nchemba.


Nae Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya zaidi ya taa 400 zitawekwa katika daraja la Pangani na mitaa yake ili kupendezesha mji huo na hivyo kuchochea utalii.

Amesema Serikali iko katika hatua za mwisho kujenga barabara ya Kwamsisi-Mkata km 38 ili kuiunganisha barabara ya Pangani-Bagamoyo na Segera-Chalinze na hivyo kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi mkoani Tanga na kuleta tija kwa bandari ya Tanga.

Eng. Kasekenya ametaja mikakati mingine ya Serikali kuwa ni pamoja na kujenga barabara ya Boza-Muheza, Tanga Bypass km 63 na barabara ya Mabokweni- Maramba-Kwamndolwa hadi Old Korogwe km 127 ili kuhakikisha jiji la Tanga linafikika kwa njia nyingi na kupunguza msongamano.

" Lengo la Serikali ni kuwa na miundombinu bora itakayochochea utalii wa pwani ya Tanga na kukuza uchumi wa mkoa na watu wake", amesisitiza Eng. Kasekenya.

Barabara ya Tanga-Pangani Mkange-Tungamaa ni sehemu ya barabara kuu ya Afrika Mashariki yenye urefu wa km 454 inayounganisha Tanzania na Kenya kuanzia Mombasa- Lungalunga- Horohoro -Tanga- Pangani-Kwamsisi hadi Mkange hivyo kukamilika kwake kutachochea uchumi na kukuza ajira na utalii kwa wananchi wa ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment