Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Kamishna wa Polisi (CP) Mhe. Suzan Kaganda, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ethiopia nchini Zimbabwe, Mhe. Rashid Mohammed Abdulwahid, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Kaganda aliishukuru Serikali ya Ethiopia kwa kuendelea kudumisha urafiki wa muda mrefu na Tanzania, huku akisisitiza kuwa uhusiano huo ulianzishwa na waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na Hayati Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia.
Balozi Kaganda ameipongeza Ethiopia kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni 2026, akieleza kuwa Tanzania ni mshirika wa karibu wa Ethiopia, ambapo amewatakia wananchi wa nchi hiyo amani, umoja na mshikamano katika kipindi chote cha uchaguzi huo.
Kwa upande wake, Balozi Abdulwahid amemshukuru Balozi Kaganda kwa kutenga muda wake kwa ajili ya mazungumzo hayo huku akibainisha kuwa hatua hiyo si tu ishara ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili, bali pia inaonesha namna Tanzania na Ethiopia zinavyoendelea kuthamini misingi ya kindugu iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo.
Vilevile, alieleza kuwa anatambua mchango unaotolewa na Tanzania kwa Ethiopia katika majukwaa ya kikanda na kimataifa, ikiwemo kuunga mkono jitihada za nchi hiyo katika kuwania nafasi mbalimbali katika taasisi na majukwaa hayo.
Katika hatua nyingine, Balozi Kaganda alitembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Indonesia nchini Zimbabwe kwa ajili ya kutoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Makamu wa Rais Mstaafu wa Indonesia, Jenerali Mstaafu Try Sutrisno, aliyefariki dunia tarehe 02 Machi 2026.
Ziara hiyo ilikuwa ni ishara ya mshikamano na kuendeleza mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Indonesia.





No comments:
Post a Comment