
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amepokea ugeni na mwaliko kutoka kwa Mwigizaji maarufu wa vichekesho nchini, Konjesta John maarufu kwa jina la "Mama Mawigi" aliyefika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam.
Mwigizaji huyo alifika kwa Waziri huyo kwa lengo la kuunga mkono andiko la ubunifu (Ubunifu Challenge) kwa wanafunzi wa uhandisi wa vyuo vikuu lililoanzishwa na Waziri huyo ili kutatua changamoto ya foleni kwa jiji la Dar es Salaam.
Pia, Mwigizaji huyo alifika kumpa mwaliko Waziri huyo kuhudhuria tamasha lake la vichekesho lililopangwa kufanyika Machi 6 mwaka huu, ambapo amesema atatumia sanaa ya ucheshi kufikisha ujumbe wake kwa jamii kuhusu namna ya kutatua kero za foleni mijini.
Katika hatua nyingine, Ulega amepokea ujumbe kutoka kwa Serikali ya Wanafunzi wa UDSM (DARUSO) na Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET) ambapo amewashukuru wanafunzi na mwitikio wa Watanzania kwenye suala hilo.
“Nashukuru kuona andiko la ubunifu challenge limepokewa vema. Mpaka wasanii wa ucheshi nao wanatoa ushauri. Wanafunzi mpaka wa shule ya msingi nao wametoa maoni yao. Inbox zangu zimejaa maoni. Kwa kweli Watanzania wanaipenda nchi yao", ameeleza Ulega.
Amefafanua kuwa Serikali ina mipango na wataalamu wake na lengo la kuanzisha zoezi hilo kwa wanafunzi kukuna vichwa vyao kuhusu changamoto iliyopo katika jiji la Dar es Salaam lilikuwa ni kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uwezeshaji wa vijana nchini.
Itakumbukwa Mwishoni mwa mwezi Februari, 2026 akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri Ulega alitangaza donge nono la Shilingi Milioni 10 kwa wanafunzi watakaoibua mawazo ya kibunifu yatakayotatua kero za Watanzania yakiwemo masuala kama ya foleni, nyumba za gharama nafuu na barabara za vijijini.



No comments:
Post a Comment