WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI SHULE YA AMALI MKOANI RUKWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, March 9, 2026

WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI SHULE YA AMALI MKOANI RUKWA


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Jumatatu, Machi 9, 2026 ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Amali ya Mkoa wa Rukwa iliyopo katika Kata ya Majengo, Namanyere, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.

Mradi huo unatekelezwa kupitia Programu ya Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6 na unalenga kuboresha elimu ya ufundi stadi kwa kuwaandaa wanafunzi kupata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuchangia maendeleo ya kiuchumi ya Taifa.

Mradi huo ulianza kutekelezwa Desemba 20, 2024 na ulitarajiwa kukamilika Machi 30 2025, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimetumika katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, hadi sasa ujenzi wa madarasa nane pamoja na jengo la utawala umekamilika na miundombinu hiyo tayari inatumika. Pia ujenzi wa jengo la TEHAMA na maktaba, nyumba ya mtumishi pamoja na vyoo vya wavulana na wasichana umekamilika na miundombinu hiyo imeanza kutumika.

Halikadhalika, ujenzi wa miundombinu mingine unaendelea katika hatua mbalimbali ikiwemo karakana ya uashi ambayo ipo katika hatua ya ufungaji wa mfumo wa umeme, karakana ya ufundi magari na mitambo iliyo katika hatua ya sakafu na ufungaji wa umeme pamoja na mabweni manne ambapo matatu yako katika hatua ya dari na moja katika hatua ya sakafu na dari.

Miundombinu mingine inayoendelea kujengwa ni jengo la maabara ambalo lipo katika hatua ya ufungaji wa mfumo wa maji na sakafu, bwalo la chakula ambalo lipo katika hatua ya kupiga sakafu pamoja na kufunga madirisha na milango, pamoja na tanki la maji ambalo linaendelea kuunganishwa na huduma ya maji kutoka NAUWASA.

Katika utekelezaji wa mradi huo, wananchi wa eneo hilo wamechangia nguvu zao kwa kutoa eneo la ekari 38 lenye thamani ya shilingi milioni 38, pamoja na kuachia boma la vyumba vitatu vya madarasa lenye thamani ya shilingi milioni 20, hivyo kufanya jumla ya mchango wa wananchi kufikia shilingi milioni 58.

No comments:

Post a Comment