Katibu Mkuu Mteule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (Anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki) Mhe. Balozi Stephen Mbundi, amekipongeza kikundi cha wanawake cha wizara hiyo, ‘Nje Women’, kwa uimara wake katika kuimarisha ushirikiano na kusaidiana kwenye masuala ya kijamii.
Balozi Mbundi ametoa pongezi hizo jijini Dodoma wakati akihutubia kama Mgeni Rasmi katika hafla maalum ya kuwaaga watumishi wanawake wa wizara hiyo wanaostafu utumishi wa umma. Amekisisitiza kikundi hicho kuanzisha Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), ili kuwakwamua wanachama wake kiuchumi na kujijengea uimara wa kifedha hata baada ya kumaliza muda wao wa utumishi serikalini.
Aidha amewaasa wastaafu walioagwa kuona kuwa kustaafu sio laana au adhabu bali ni mwanzo wa kuendelea kufanya kazi na kuanzisha miradi mingine ambayo haihusiani na utumishi wa umma.
Akizungumza kwa njia ya mtandao, Mhe. Balozi Mstaafu Fatma Rajab alielezea uzoefu wake wa maisha ya kustaafu, akisisitiza umuhimu wa kujiandaa kisaikolojia na kifedha ili kuendelea kuishi maisha yenye staha na tija nje ya ofisi. Ili kuwajengea uelewa wa masuala ya kifedha, hafla hiyo ilihusisha mada kutoka kwa wataalamu wa uwekezaji wa taasisi ya UTT na Hazina SACCOS, ambao walielezea umuhimu wa kuwekeza mapema.
Nao wastaafu waliofanyiwa sherehe hiyo wameishukuru Wizara na kikundi cha ‘Nje Women’ kwa kuonesha upendo na kuthamini mchango wao kazini, huku wakihimiza watumishi waliobakia kazini kujiwekea akiba mapema kama maandalizi bora ya kustaafu. Sherehe hiyo yenye tukio la kihistoria imehitimishwa kwa kutoa wito kwa wanawake wote wizarani hapo kuendelea kushirikiana na kudumisha umoja wao.















No comments:
Post a Comment