Na OWM - TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amesema Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi utaleta mabadiliko ya kweli kwa kubadilisha eneo la bonde la msimbazi ambalo ni hatarishi kwa sasa na kuwa sehemu muhimu kwa uchumi na mazingira ya Dar es Salaam.
Prof. Shemdoe amesema hayo Aprili 20, 2026 jijini Dar es Salaam, katika hafla ya Utiaji Saini mkataba huo wa Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini humo.
Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi huo utanusuru maisha ya jamii kwa kuhamisha zaidi ya nyumba 3,000 kutoka maeneo hatarishi kwa mafuriko na kutoa fidia stahiki, na kuongeza kuwa Serikali itahakikisha kunakuwa na usalama na ustawi wa wananchi wa eneo ambalo mradi unajengwa.
“Mradi utawezesha upatikanaji wa hekta 57 za ardhi salama iliyotengenezwa, ambayo itatoa maeneo mapya kwa ajili ya makazi na biashara na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na kutengeneza ajira,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, mradi utaboresha miundombinu kupitia ujenzi wa daraja jipya la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na karakana mpya ya mabasi ya mwendokasi eneo la Ubungo Maziwa ambapo miundombinu hiyo kwa kiasi kikubwa itaboresha usafiri na muingiliano ndani ya jiji.
Prof. Shemdoe ameanisha kuwa, mradi huu ulianza kufikiliwa mwaka 2018 na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais pindi yalipotokea mafuriko na maafa makubwa kwenye Bonde la Mto Msimbazi, alipoamua kuitisha kikao cha watendaji wa wizara zinazohusika ili kujadiliana namna ya kutokomeza kabisa mafuriko yanayotokea katika Bonde la Msimbazi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff amesema kuwa, mradi utajenga daraja jipya eneo la Jangwani lenye urefu wa mita 390 pamoja na karakana mpya ya mabasi ya mwendokasi katika eneo la Ubungo Maziwa na kuongeza kuwa mradi utaboresha maeneo korofi katika eneo la juu la bonde pamoja na kuratibu shughuli za kibinadamu ili kudhibiti mmomonyoko wa udongo ambao husababisha mafuriko.
Mradi ulianza rasmi mwezi Februari 2023 na utatekelezwa kwa muda wa miaka sita, kwa gharama inayokadiriwa kuwa Dola za Marekani Milioni 260 zinazotokana na mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (Dola Milioni 200), mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya Uhispania (Dola Milioni 30) na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi (Euro Milioni 30).












No comments:
Post a Comment