RC HAMIDA AIBUA MKAKATI MPYA WA KUVUTA WATALII ZANZIBAR KWENDA MIKUMI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 15, 2026

RC HAMIDA AIBUA MKAKATI MPYA WA KUVUTA WATALII ZANZIBAR KWENDA MIKUMI


Na Mwandishi Wetu, Mikumi-Morogoro


Katika hatua mpya ya kuimarisha sekta ya utalii nchini, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Hamida Mussa Hamis, amebainisha mkakati wa kipekee wa kuendelea kuwavutia watalii wanaotembelea Zanzibar kuongeza safari zao kwa kutembelea vivutio vya Tanzania Bara, hususan Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kutokana na upekee wake 


Akizungumza baada ya kutembelea hifadhi hiyo iliyopo mkoani Morogoro, Mhe. Hamida amesema ipo haja ya kutumia fursa ya wingi wa watalii wanaoendelea kumimina Zanzibar kama daraja la kuutangaza utalii wa Bara ikiwemo hifadhi za taifa kama Mikumi.

“Zanzibar ni lango kubwa la utalii, lakini tunataka wageni hawa wasiishie visiwani pekee bali wavuke na kuja kuona hazina ya vivutio tulivyonavyo Bara,” amesema.

Katika kile alichokiita uzoefu wa kipekee, Mhe. Hamida alieleza kufurahishwa na tukio la kuona simba ndani ya muda mfupi mara tu baada ya kuingia hifadhini hapo, Tena wakiwa chini ya Ndege zilizoegeshwa ndani ya hifadhi zinazotumika kuleta wageni Mikumi kutokea Zanzibar akisema hali hiyo inaonesha ubora wa vivutio vya Tanzania.

Ameongeza kuwa miundombinu iliyopo ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, usafiri wa anga na barabara pamoja na miundo mbinu mizuri ya ndani inayofikika kirahisi licha ya Mvua, imeifanya Mikumi kuwa miongoni mwa hifadhi bora zinazofikika kirahisi kwa watalii wa ndani na nje.

Katika hatua nyingine, aliwahimiza Wazanzibari kubadili mtazamo na kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya ndani, akisisitiza kuwa utalii si wa wageni pekee bali ni fursa kwa Watanzania wote.

“Ni wakati sasa kwa Watanzania kuwekeza katika kujitambua na kuthamini vivutio vyetu; utalii wa ndani ni msingi imara wa sekta hii,” amesisitiza.

Aidha akawahimiza watanzania kutokea Upande wa Bara kutembelea vivutio vya Utalii wa Zanzibar ikiwemo utalii wa fukwe, kuogelea na dolphins na matamasha mbalimbali likiwemo la Kizimkazi ili kufurahia upekee uliopo.

"Hata Rais wetu Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar Dkt Husein Ali Mwinyi, wanahimiza utalii wa Ndani, Rais Samia alifanya Kazi kubwa kutangaza Royal Tour, tuwaunge mkono kivitendo viongozi wetu"Amesisitiza.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Augustine Masesa, alifichua kuwa idadi kubwa ya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo wanatoka Zanzibar.

Amesema hali hiyo inaashiria mafanikio ya juhudi za kuitangaza Tanzania kupitia kampeni mbalimbali ikiwemo Royal Tour, huku akibainisha kuwa bado kuna fursa kubwa zaidi ya kuongeza idadi hiyo kupitia ushirikiano wa pande zote mbili.

Amesisitiza kuwa Mikumi inaendelea kuwa kivutio muhimu kinachochochea utalii wa ndani na wa kimataifa, huku akiwakaribisha Watanzania na wageni kufika kujionea vivutio hivyo kwa macho yao wenyewe hasa kutokana na miundo mbinu Rafiki na inayofikika kirahisi ikiwemo Reli ya SGR, Barabara na ndege ambazo kutoka Zanzibar ni dakika 40 tu kufika.

No comments:

Post a Comment