Serikali imesema imetenga kiasi cha shilingi bilioni 52.25 katika bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa ajili ya kuzifanyia ukarabati hospitali za Wilaya na Manispaa 105, ikiwa ni mkakati wa kuboresha miundombinu ya hospitali hizo nchi nzima.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Jafar Seif, katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mpanda Mjini, Mhe. Haidary Sumry, aliyetaka kujua ni lini Hospitali ya Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi itapata jengo la dharura.
Katika majibu yake, Naibu Waziri Dkt. Seif amesema Serikali inatambua upungufu wa majengo pamoja na uchakavu wa baadhi ya majengo katika hospitali mbalimbali nchini, ndiyo maana imeweka mpango kwa kutenga kiasi hicho cha fedha kitakachoelekezwa katika ukamilishaji wa baadhi ya miundombinu muhimu ili kuwezesha utolewaji wa huduma za afya kwa jamii.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha majengo hayo, na kusisitiza kuwa vituo vya afya ambavyo bado ujenzi wake haujakamilika ni vyema wataalamu wakaanza kutoa huduma za msingi kupitia majengo yaliyopo, kama vile matibabu kwa wagonjwa wa nje (OPD), ili kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu kwa jamii.


No comments:
Post a Comment