Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb) tarehe 11 Aprili, 2026, katika jimbo dogo la Mara Kaskazini wilayani Tarime, mkoani Mara amemuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt Mwigulu Lameck Nchemba katika Harambee ya kuchangia ujenzi wa ofisi za mkoa za jimbo la Kanisa la Waadvertista wa Sabato.
Akiwasilisha salamu za Mhe Waziri Mkuu, kwa wananchi na waumini wa kanisa hilo mkoani Mara, Mhe Dkt Rhimo Nyansaho amesema Mheshimiwa Waziri Mkuu anawapongeza Waumini na viongozi wa kanisa hilo kwa hatua ya ujenzi wa Ofisi za mkoa na amepokea kwa heshima mwaliko wa kuwepo kwenye harambee hiyo, lakini kutokana na majukumu ya kitaifa ameshindwa kuwa pamoja nao katika shughuli hiyo muhimu ya kijamii na kiimani.
Waziri Mkuu, Mhe Dkt Mwigulu Nchemba katika salamu zake kwa waumini wa kanisa hao,amewapongeza kwa moyo wa kujitolea walio nao katika kuendeleza kazi ya Mungu.
Akaeleza kuwa taasisi za dini zina mchango mkubwa sana katika kujenga maadili, mshikamano wa kijamii, na amani katika Taifa la Tanzania.
Katika Harambee hiyo iliyoongozwa na Mheshimiwa Dkt Rhimo Nyansaho,zaidi ya shilingi milioni 630 zilichangwa na wadau mbalimbali wa kanisa hilo wakiwemo watu na mashirika binafsi pamoja na wananchi.









No comments:
Post a Comment