
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali imezindua mabasi maalum matatu kwa ajili ya kuwahudumia watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hatua inayolenga kupunguza changamoto za usafiri na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Prof. Daniel Mushi, amesema serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kazi kwa watumishi wa umma ili kuongeza tija na ufanisi.

Prof. Mushi, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Prof. Carolyne Nombo, ameeleza kuwa uwekezaji huo unaakisi dhamira ya serikali ya kuthamini mchango wa watumishi wa umma, huku akiwataka kutumia fursa hiyo kuongeza uwajibikaji na kuchangia maendeleo ya taifa.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuyatunza mabasi hayo kwa kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa na kuyafanyia matengenezo ya mara kwa mara ili yadumu na kuendelea kutoa huduma bora.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Dkt. Edith Rwiza, amesema tangu kuhamia Mtumba, watumishi walikumbwa na changamoto kubwa ya usafiri iliyowalazimu kutumia kati ya shilingi 10,000 hadi 15,000 kwa siku, hali iliyoathiri ustawi wao na kushusha morali ya kazi.
Amefafanua kuwa wizara ilitenga bajeti katika mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya ununuzi wa mabasi hayo kupitia programu ya BOOST, ambapo mchakato ulianza Julai 2025 na kukamilika Machi 2026. Mabasi hayo yamenunuliwa kupitia Shirika la Kimataifa la UNOPS kwa gharama ya shilingi milioni 550.8.














No comments:
Post a Comment