WIZARA YA MAWASILIANO YAOMBA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 222.5, KIPAUMBELE KIKUBWA MIRADI YA MAENDELEO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 30, 2026

WIZARA YA MAWASILIANO YAOMBA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 222.5, KIPAUMBELE KIKUBWA MIRADI YA MAENDELEO


Na Okuly Julius ,OKULY BLOG,DODOMA


Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikieleza dhamira ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.


Akiwasilisha bajeti hiyo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah  Kairuki, amesema wizara inakadiria kukusanya jumla ya Shilingi 160,369,240,000, fedha zitakazotokana na mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.


Alieleza kuwa makusanyo hayo yanatarajiwa kuongezeka kutokana na kuimarika kwa matumizi ya huduma za mawasiliano, pamoja na upanuzi wa miundombinu ya mkongo unaoendelea kufanyika nchini na katika ukanda wa kikanda.


Kwa upande wa matumizi, Waziri Kairuki aliomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi 222,589,451,000 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu na vipaumbele vya wizara hiyo katika mwaka ujao wa fedha.


Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi 13,146,172,000 sawa na asilimia 5.9 ya bajeti yote, zitatumika kwa matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo, Shilingi 6,371,830,000 zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, huku Shilingi 6,774,342,000 zikitengwa kwa matumizi mengineyo ya uendeshaji wa wizara.


Aidha, sehemu kubwa ya bajeti hiyo, kiasi cha Shilingi 209,443,279,000 sawa na asilimia 94.1, imetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, jambo linaloonesha msisitizo wa serikali katika uwekezaji wa miundombinu ya TEHAMA.


“Kati ya fedha za maendeleo, Shilingi 98,480,905,000 ni fedha za ndani na Shilingi 110,962,374,000 ni fedha kutoka vyanzo vya nje, zitakazowezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati,” alisema Waziri Kairuki.


Alisisitiza kuwa uwekezaji huo utaongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi, kuboresha huduma za intaneti, na kuwezesha maendeleo ya sekta nyingine kupitia matumizi ya teknolojia.


Waziri Kairuki aliongeza kuwa bajeti hiyo inalenga kuendeleza mageuzi ya kidijitali, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma, na kuchochea ukuaji wa uchumi unaotegemea maarifa na teknolojia, sambamba na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ushindani wa kidijitali kikanda na kimataifa.

No comments:

Post a Comment