Na Okuly Julius ,OKULY BLOG ,DODOMA
Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
imeendelea kuonesha ukuaji mkubwa nchini, huku ongezeko la watumiaji wa huduma
mbalimbali za kidijitali likidhihirisha mafanikio ya uwekezaji unaoendelea
kufanywa na Serikali.
Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Alisema idadi ya laini za simu zilizosajiliwa imeongezeka
kutoka milioni 90.4 Machi 2025 hadi kufikia milioni 111.9 Machi 2026, sawa na
ongezeko la asilimia 23.8.
Alisema sambamba na hilo, matumizi ya intaneti
yameendelea kupanuka ambapo watumiaji wameongezeka kutoka milioni 49.3 hadi
milioni 58.9 katika kipindi hicho, sawa na ongezeko la asilimia 19.5.
Kwa upande wa huduma za fedha kwa njia ya simu,
Waziri Kairuki alibainisha kuwa watumiaji wameongezeka kutoka milioni 66.5 hadi
milioni 81.0, sawa na ongezeko la asilimia 21.8, hali inayoonesha kuimarika kwa
matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali nchini.
“Takwimu hizi zinaonesha wazi jinsi wananchi
wanavyozidi kuamini na kutumia huduma za TEHAMA katika maisha yao ya kila siku,
hususan katika mawasiliano, biashara na huduma za kifedha,” alisema Waziri
Kairuki.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alieleza
kuwa idadi ya watoa huduma wa miundombinu ya mawasiliano imeongezeka kutoka 38
Machi 2025 hadi kufikia 52 Machi 2026, sawa na ongezeko la asilimia 36.8, jambo
linaloashiria kuimarika kwa ushindani na uwekezaji katika sekta hiyo.
Aidha, watoa huduma za ziada (Application
Services na Value-Added Services) wameongezeka kutoka 136 hadi 173 katika
kipindi hicho, sawa na ongezeko la asilimia 27.2, hatua inayochochea ubunifu na
upatikanaji wa huduma mbalimbali za kidijitali.
Waziri Kairuki alisisitiza kuwa mafanikio hayo
yanatokana na uwepo wa mifumo na mazingira wezeshi yaliyojengwa na Serikali
chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yenye lengo la kuhakikisha huduma za
mawasiliano zinawafikia wananchi wengi zaidi mijini na vijijini.
Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji katika TEHAMA ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za kidijitali, sambamba na kukuza uchumi wa taifa unaotegemea teknolojia na ubunifu.


No comments:
Post a Comment