Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Michezo na Utamaduni, Husna Sekiboko amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kutumia ujuzi uliopo kwa vijana katika kujenga uchumi wa uzalishaji, badala ya kuendelea kutegemea bidhaa kutoka nje.
Sekiboko ameyasema hayo leo Agosti 19,2026 baada ya kutembele maandalizi ya mashindano ya ujuzi yatakayoanza kesho Agosti 20 ikiwa ni sehemu muendelezo wa maonesho ya kitaifa ya wiki ya elimu, ujuzi na ubunifu yanayoendelea katika katika viwanja vya Shule ya sekondari Usagara Jijini Tanga
Ametolea mfano katika eneo la ufundi wa magari, ambako baadhi ya washiriki wameonesha uwezo wa kubuni na kutengeneza vipuri ambavyo kwa sasa sehemu kubwa huagizwa kutoka nje ya nchi.
“Baadae wakiweza kuunganishwa na soko na wakaanza kuzalisha vile vipuli, hata soko la vipuli nchini litakuwa limepungua,” amesema Sekiboko.
Amesema fursa hiyo pia ipo katika sekta nyingine, ikiwemo ujenzi na ushonaji, ambako vijana wameonesha uwezo wa kutengeneza bidhaa zenye ubora na zinazoweza kushindana sokoni.
Kwa upande wa mavazi, Sekiboko amesema ubunifu unaooneshwa na washiriki unaweza kuifanya Tanzania kufikia hatua ya kuzalisha nguo zenye viwango ndani ya nchi na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoingizwa kutoka mataifa kama Uturuki na China.
“Ujuzi mnao ubuni leo unaweza kuchukuliwa kama ni wazo, lakini kesho inaweza kuwa ni bidhaa ambayo mnaiuza, ujuzi wako unaweza kuwa ni biashara,” amesema.
Kwa mujibu wa Sekiboko, amesema kinachohitajika kwa sasa ni kuwaunganisha wabunifu na masoko pamoja na kuwawezesha kupata mitaji ili mawazo yao yaweze kubadilishwa kuwa bidhaa zinazozalishwa kwa kiwango kikubwa.
"Hatua hiyo inaweza kuwa na manufaa kwa vijana binafsi kwa kuwawezesha kujiajiri na kuongeza kipato, lakini pia kwa taifa kupitia uzalishaji wa bidhaa, ajira na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje,"amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa WorldSkills kutoka Ubelgiji, Philippe Kever, amesema ameridhishwa na maandalizi ya mashindano hayo huku akibainisha kuwa licha ya Tanzania kushiriki kwa mara ya kwanza na kutambuliwa rasmi katika mashindano hayo, hatua iliyofikiwa ni nzuri, huku akiwataka wasimamizi kuendelea kuboresha mashindano hayo na kujiandaa kwa mashindano yajayo.
"Uzoefu unaopatikana kupitia mashindano hayo unaweza kuisaidia Tanzania kuimarisha mifumo ya kukuza na kuendeleza ujuzi wa vijana na kuwapa nafasi zaidi ya kutumia vipaji vyao katika uzalishaji na ajira,"amesema.








No comments:
Post a Comment