ASILIMIA 85.2 YA WANANCHI VIJIJINI WAFIKIWA NA MAJI SAFI, HUDUMA ZAIDI ZAIMARIKA NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 5, 2026

ASILIMIA 85.2 YA WANANCHI VIJIJINI WAFIKIWA NA MAJI SAFI, HUDUMA ZAIDI ZAIMARIKA NCHINI




Na,Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA


Upatikanaji wa huduma ya maji vijijini umefikia asilimia 85.2 mwezi Desemba 2025 kutoka asilimia 83.1 mwezi Desemba 2024, kufuatia kukamilika kwa miradi 54 yenye vituo vya kuchotea maji 946, iliyonufaisha wananchi wapatao 493,932 nchini.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi 858 ya maji vijijini katika hatua mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo.

Amesema miradi hiyo inatekelezwa katika kanda tofauti, ikiwemo Nyanda za Juu Kusini, Kusini, Kaskazini, Mashariki, Ziwa na Magharibi, ambapo baadhi yake ni mradi wa Ihalimba, Ifwagi na Ikongosi (Iringa), mradi wa maji kutoka Mto Nyangao kwa Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Lindi, pamoja na miradi ya Mkinga–Horohoro (Tanga) na Dambia–Hydom (Manyara).

Katika kuimarisha uendelevu wa huduma za maji vijijini, Aweso amesema Wizara imevisajili na kuviwezesha Vyombo vya Watumiaji Maji ngazi ya Jamii (CBWSOs), ambapo hadi Aprili 2026 jumla ya vyombo 918 vimesajiliwa na kuajiri wataalam 6,728. Aidha, vyombo 914 vimeunganishwa na mfumo wa GePG ili kuongeza uwazi na nidhamu ya matumizi ya fedha.

Kwa upande wa mijini, Aweso amesema upatikanaji wa majisafi umeongezeka kutoka asilimia 90.6 mwezi Desemba 2024 hadi asilimia 92.5 mwezi Desemba 2025, kutokana na utekelezaji wa miradi 226 ya maji mijini.

Amesema hadi Aprili 2026, miradi 12 imekamilika huku mingine 214 ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ambapo 16 kati yake imefikia zaidi ya asilimia 95 na tayari inatoa huduma kwa wananchi.

Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ule wa usambazaji maji katika maeneo ya nje ya mtandao katika Manispaa za Kigamboni, Temeke na Ilala, mradi wa kuboresha huduma ya maji kutoka Bwawa la Mindu mkoani Morogoro, pamoja na miradi ya maji katika miji ya Dodoma, Mwanza, Arusha, Mbeya, Njombe na Songwe.

Kuhusu usafi wa mazingira, Aweso amesema Serikali imeendelea kupanua miundombinu ya majitaka mijini, ambapo urefu wa mtandao umeongezeka kutoka kilomita 1,513.11 hadi 1,598.88, huku idadi ya wateja waliojiunga na huduma hiyo ikifikia 61,313.

Ametaja miradi muhimu inayotekelezwa kuwa ni pamoja na mradi wa majitaka Manispaa ya Musoma, mradi wa Area C na D jijini Dodoma, pamoja na ujenzi wa mtambo wa kuchakata majitaka Mbezi Beach jijini Dar es Salaam na mabwawa ya kutibu majitaka katika mji wa Babati.

Aweso amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha huduma za maji na usafi wa mazingira ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na endelevu nchini.

No comments:

Post a Comment