WIZARA YA MAJI YAJA NA VIPAUMBELE 7 KUBORESHA HUDUMA YA MAJI NCHINI 2026/27 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 5, 2026

WIZARA YA MAJI YAJA NA VIPAUMBELE 7 KUBORESHA HUDUMA YA MAJI NCHINI 2026/27



Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA

 

Usalama wa maji kwa matumizi ya kijamii na kiuchumi umepewa kipaumbele kikuu katika mwaka wa fedha 2026/2027, huku Serikali ikilenga kutumia rasilimali hiyo kama kichocheo cha mageuzi ya uchumi kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Wizara imeweka mikakati mahsusi kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa wa uhakika na endelevu nchini.

Aweso amesema miongoni mwa vipaumbele vikuu ni kukamilisha maandalizi ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Maji (National Water Master Plan) ambao utatoa mwongozo wa muda mrefu wa usimamizi, matumizi na uwekezaji katika rasilimali za maji.

Aidha, amesema Serikali itaendelea na utekelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji (National Water Grid), unaolenga kuunganisha vyanzo vikuu vya maji ikiwemo maziwa, mito mikubwa na mabwawa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote ya nchi.

Katika utekelezaji huo, Wizara imekamilisha usanifu wa mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Dodoma kupitia Singida, huku ikiendelea na usanifu wa miradi ya maji kutoka Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, pamoja na mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji kupeleka Dar es Salaam na mkoa wa Pwani.

Kwa upande wa uvunaji wa maji ya mvua, Aweso amesema Wizara imepanga kujenga na kukarabati mabwawa 33, kufanya usanifu wa mabwawa mapya 34, pamoja na kuchimba visima virefu 300 katika maeneo yenye uhaba wa maji.

Katika kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma, Wizara imepanga kukamilisha miradi 992 ya maji vijijini, miradi 196 ya maji mijini pamoja na miradi 26 ya usafi wa mazingira, hatua itakayosaidia wananchi kunufaika kwa wakati na uwekezaji wa Serikali.

Aweso amesema Serikali pia itaanza utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 314 ambavyo bado havina huduma, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kufikia vijiji 1,575 ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo.

Katika kudhibiti upotevu wa maji, Wizara itaongeza matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo mifumo ya usomaji mita kwa njia ya kielektroniki na ufuatiliaji wa mitandao ya maji, sambamba na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waharibifu wa miundombinu na wizi wa maji.

Aidha, Wizara imeweka kipaumbele katika kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira katika vituo vya afya na shule, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma hizo muhimu zinapatikana kwa uhakika na kusaidia kulinda afya za wananchi.

Aweso amesisitiza kuwa utekelezaji wa vipaumbele hivyo utaenda sambamba na kuimarisha usimamizi wa miradi, matumizi bora ya fedha za umma na kuhakikisha huduma za maji zinakuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

No comments:

Post a Comment