Na Mwandishi Wetu , Dodoma.
Tanzania inatarajia kutumia matukio ya kimataifa yatayofanyika hapa nchini kwa lengo la kutangaza fursa za utalii zilizopo nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameyasema hayo Bungeni Mjini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Ameongeza kuwa, Tanzania inatarajia kutumia fursa za matukio manne yatakayofanyika hapa nchini ili kutangaza vivutio vya utalii nchini.
Ameyataja matukio hayo kuwa ni Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (Inter Parliamentary Union Assembly-(IPU), utakaofanyika mwezi Oktoba 2026 jijini Arusha ambapo zaidi ya washiriki 1,500 na Maspika 183 kutoka nchi mbalimbali Duniani watahudhuria, tukio la utoaji wa tuzo za kimataifa za ubora kwenye sekta ya utalii duniani litakalofanyika mwezi Desemba mwaka 2026 ambapo washiriki zaidi ya 1,000 kutoka mabara ya Ulaya, Asia, Amerika ya kaskazini na kusini watahudhuria.
Matukio mengine ni Shindano la Ulimbwende wa Dunia 2027 (Miss World) ambalo litahudhuriwa na takribani watu 20,000 pamoja na washindani 120 kutoka nchi mbalimbali Duniani na Mashindano ya mpira wa miguu kwa nchi za Afrika (AFCON 2027) ambapo Tanzania inatarajia kupokea wageni zaidi ya Milioni 1.8 na kuhusisha timu 24 kutoka Mataifa ya Afrika.
Dkt. Kijaji ameongeza kuwa Wizara imejipanga kikamilifu kutumia fursa za matukio hayo kutangaza vivutio vya utalii vilvyopo nchini kwa kushirikiana na wadau wa utalii kuandaa vifurushi maalumu vya safari za utalii kwa wageni watakaofika nchini kwa ajili ya matukio hayo ya kimataifa.



No comments:
Post a Comment