SERIKALI YASISITIZA ASILIMIA 10 YA MAPATO YA TAKA KUREJESHWA KWENYE VITENGO VYA UDHIBITI TAKA. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 12, 2026

SERIKALI YASISITIZA ASILIMIA 10 YA MAPATO YA TAKA KUREJESHWA KWENYE VITENGO VYA UDHIBITI TAKA.



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, amezielekeza halmashauri zote nchini kutenga na kurejesha asilimia 10 ya mapato yatokanayo na shughuli za udhibiti wa taka kwa ajili ya kuimarisha vitengo vya usafi wa mazingira na udhibiti wa taka.

Profesa Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo Mei 12, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Utekelezaji wa Afua za Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafi wa Miji uliobebwa na kaulimbiu isemayo “Taka Ngumu ni Mali; Tumia, Rejeleza na Weka Miji Safi.”

Amesema kati ya halmashauri 184 nchini, halmashauri 43 pekee ndizo zenye maeneo maalum ya kutupia taka, hali inayohitaji hatua za haraka kwa halmashauri ambazo bado hazijaanzisha madampo rasmi.

“Bado baadhi ya halmashauri hazina maeneo rasmi ya kutupia taka, hali inayodhoofisha juhudi za usafi na uhifadhi wa mazingira. Ni muhimu kuhakikisha taka zinakusanywa katika maeneo maalum ili miji yetu ibaki safi,” amesema Profesa Shemdoe.

Aidha, amewataka wakuu wa mikoa, wilaya pamoja na viongozi wa serikali za mitaa kuhakikisha suala la usafi wa mazingira linakuwa agenda ya kudumu katika vikao vya maamuzi kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji na mitaa.

Amesema utupaji holela wa taka kwenye mitaro ya maji ni chanzo kikubwa cha mafuriko wakati wa mvua kutokana na kuziba njia za maji.

“Madhara ya kutupa taka ngumu kwenye mitaro ya maji husababisha maji kukosa mwelekeo na kuingia katika makazi ya wananchi. Wajibu wa kudhibiti hali hiyo ni wa viongozi na vitengo vya usafi kwa kushirikiana na jamii,” amesema.

Profesa Shemdoe pia ameitaka jamii kubadili mtazamo kuhusu taka na kuziona kama rasilimali yenye uwezo wa kuongeza kipato na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Amesema hatua hiyo itawezekana kupitia mfumo madhubuti wa kutenganisha taka kuanzia zinakozalishwa ili kurahisisha urejelezaji wa plastiki, vyuma, karatasi na taka nyingine zinazoweza kutumika tena.

“Tumekubaliana kuwa taka ni mali, hivyo ni lazima tuziongezee thamani kwa kuanza kuzitenganisha kuanzia maeneo zinakozalishwa. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeongeza thamani ya taka na kuimarisha uchumi wa wananchi,” amesema.

Kadhalika, amewahimiza vijana na wanawake kutumia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kuanzisha shughuli za ukusanyaji na uchakataji wa taka ngumu ili kujiongezea kipato huku wakichangia usafi wa mazingira.

“Taka kama chupa za plastiki zinaweza kuuzwa kwa kampuni zinazofanya urejelezaji na hivyo kuwa chanzo cha ajira na mapato kwa wananchi,” amesema.

Profesa Shemdoe amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo, ikiwemo Japan, kutafuta teknolojia za kisasa za uteketezaji na urejelezaji wa taka ngumu.

Amesema tayari kuna mpango wa majaribio ya matumizi ya teknolojia hizo katika baadhi ya miji nchini kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu la usimamizi wa taka.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Mkoa wa Dodoma umeongeza bajeti ya usafi wa mazingira kutoka Sh milioni 750 hadi Sh bilioni 3 kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema fedha hizo zitatumika kununua vifaa vya usafi, kuimarisha ukusanyaji wa taka pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Mabadiliko ya Tabianchi na Tathmini kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Kanizio Manyika, amesema Tanzania huzalisha zaidi ya tani milioni 17 za taka ngumu kwa mwaka huku asilimia 60 hadi 75 ya taka hizo zikibaki kwenye mazingira kutokana na kutokusanywa ipasavyo.

Amesema hali hiyo ni hatari kwa afya za wananchi na mazingira, hivyo kuna haja ya kuwa na mifumo endelevu ya usimamizi wa taka ngumu.

Naye mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Joseph Birango, amesema takwimu zinaonesha kuwa magonjwa sita kati ya 10 yanayoisumbua jamii yanachangiwa na uchafuzi wa mazingira pamoja na ukosefu wa mifumo bora ya usimamizi wa taka.

“Hivyo kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu usafi wa mazingira ili kupunguza magonjwa ya mlipuko pamoja na gharama za matibabu zinazotolewa na serikali,” amesema.

Awali, Mwenyekiti wa Wakuu wa Vitengo vya Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira Tanzania Bara, William Mpangala kutoka Wilaya ya Bahi, aliiomba serikali kutoa maelekezo madhubuti zaidi kwa halmashauri kuhakikisha asilimia 10 ya mapato yatokanayo na udhibiti wa taka inarejeshwa kwenye shughuli za usafi wa mazingira.

Amesema licha ya uwepo wa maelekezo hayo, utekelezaji wake katika baadhi ya maeneo bado unasuasua na hivyo kukwamisha utoaji wa huduma za usafi wa mazingira.

No comments:

Post a Comment