
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Serikali imeweka masharti maalumu ya upatikanaji wa nyaraka za kihistoria zinazohifadhiwa na Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ikiwataka wananchi, wanafunzi na watafiti kufuata taratibu zilizowekwa ili kupata huduma hiyo.
Hayo yameelezwa leo Juni 22, 2026 na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Filimani Msiangi, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Msiangi amesema idara hiyo hupokea wanafunzi na watafiti kutoka ngazi mbalimbali za elimu kwa ajili ya kujifunza na kufanya tafiti zinazohusiana na historia ya taifa, huku taasisi zinazohitaji kufanya ziara za mafunzo zikitakiwa kuwasilisha maombi rasmi.
Aidha, amesema wananchi binafsi wanaotaka kutumia huduma za idara hiyo wanapaswa kuwa na barua ya utambulisho inayoeleza madhumuni ya kutembelea na kutumia nyaraka zilizohifadhiwa.
Amefafanua kuwa si nyaraka zote zinazoruhusiwa kutazamwa na umma, kwani kwa mujibu wa sheria, nyaraka nyingi hufunguliwa kwa matumizi ya umma baada ya miaka 30 tangu kufungwa kwake, wakati nyaraka za siri zikiendelea kulindwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Utaratibu huu unalenga kulinda usalama wa taifa na kuhakikisha nyaraka zinazotumika kwa ajili ya tafiti, elimu na rejea mbalimbali zinapatikana kwa njia sahihi bila kuathiri maslahi ya taifa,” amesema Msiangi.
Katika hatua nyingine, amesema idara hiyo inaendelea na juhudi za kuhifadhi na kurudufu nyaraka muhimu kwa mfumo wa kidijitali ili kuimarisha uhifadhi wa historia ya taifa na kurahisisha upatikanaji wake kwa vizazi vya sasa na vijavyo.






No comments:
Post a Comment