Na Mwandishi Wetu - Dodoma
ZAIDI ya wananchi 300 wametembelea banda la Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) tangu kuanza kwa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, wakipata elimu na ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara za wilaya katika maeneo yao.
Hatua hiyo imeendelea kuimarisha uhusiano kati ya wananchi na taasisi hiyo, huku ikitoa fursa ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi moja kwa moja.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma Bi. Catherine Sungura amesema wananchi wanaowasilisha kero zao huunganishwa moja kwa moja na mameneja wa maeneo husika ili kupata maelezo ya kina na ufumbuzi wa haraka.
“Tunawapokea wananchi wengi kutoka maeneo tofauti ya Tanzania ambao wengi wanataka kufahamu ujenzi au matengenezo ya barabara katika maeneo yao na hivyo wengi wao wanapata majibu hapo hapo kwani wanazungumza moja kwa moja na mameneja wa mkoa au wilaya husika”.
Amesema lengo la TARURA ni kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu miradi inayotekelezwa pamoja na hatua mbalimbali za maendeleo yake.
Bi. Sungura ametolea mfano wa mwananchi mmoja kutoka Kimara jijini Dar es Salam Bi. Sarah James Joseph ambaye amefika katika banda na kutaka kujua ujenzi wa barabara ya Kimara mwisho hadi king’ongo ujenzi wake umefikia wapi ambapo mwananchi huyo ameweza kuwasiliana na Meneja wa Wilaya ya Ubungo na kupata ufafanuzi na hivyo kupokea majibu kwa furaha na kuridhika na huduma aliyoipata kwenye banda la TARURA.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa barabara ya King'ongo iliyopo Kimara, Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Bi. Sungura amesema barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha zege kuanzia TRA kuelekea King'ong'o ambapo kilomita 1.6 pekee zimebaki na kati ya hizo, mita 800 zinatarajiwa kujengwa kuanzia Julai mwaka huu, huku sehemu iliyobaki ikikamilishwa katika awamu inayofuata.
Bi. Sungura amesisitiza kuwa TARURA itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafiri na mawasiliano kwa wananchi na kwamba barabara bora huchochea upatikanaji wa huduma za kijamii, biashara na shughuli nyingine za maendeleo, hatua inayochangia kuinua ustawi wa jamii na kukuza uchumi wa maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Bi. Sarah James Joseph mkazi wa King'ongo, Kimara jijini Dar es Salaam ameishukuru TARURA kwa kazi zao na juhudi kubwa wanazozifanya kila siku kwaajili ya kuwasaidia wananchi katika suala la mawasiliano ya barabara nchini.








No comments:
Post a Comment