TANZANIA YAPOKEA SH. BILIONI 60.7 KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI SONGWE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 22, 2026

TANZANIA YAPOKEA SH. BILIONI 60.7 KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI SONGWE


Na Mwandishi Wetu , Dodoma


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea msaada wa Euro milioni 20, sawa na Shilingi bilioni 60.7, kutoka Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira katika miji ya Tunduma na Vwawa-Mlowo, mkoani Songwe.

Msaada huo ulirasimishwa kupitia utiaji saini wa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ujerumani katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.


Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, alisema mradi huo unalenga kuboresha upatikanaji endelevu wa maji safi na salama pamoja na huduma za usafi wa mazingira kwa wakazi wa maeneo husika.

Alifafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo utahusisha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji, kuunganisha wateja wapya, kujenga mtambo wa kutibu majitaka, kununua magari ya kuvuta majitaka pamoja na kujenga miundombinu ya usafi wa mazingira katika taasisi za umma, ikiwemo vyoo katika shule zilizochaguliwa.

Dkt. Mwamba aliishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo wa Tanzania kupitia ufadhili wa miradi mbalimbali katika sekta za maji, afya, uhifadhi wa maliasili na mazingira, usimamizi wa fedha za umma pamoja na usawa wa kijinsia.

Alisema misaada hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini na kuboresha ustawi wa wananchi.

Aidha, alikumbusha kuwa katika majadiliano ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Ujerumani yaliyofanyika Machi 20, 2024 jijini Dar es Salaam, Serikali ya Ujerumani iliahidi kutoa Euro milioni 70 kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

“Fedha hizi ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi hiyo na zinaonesha kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa muda mrefu na wenye manufaa kati ya Tanzania na Ujerumani,” alisema Dkt. Mwamba.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha ushirikiano wa maendeleo na Ujerumani na kuhakikisha miradi yote inayofadhiliwa inatekelezwa kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuwanufaisha wananchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), Vanessa Eidt, alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani utaendelea kuzaa matunda kwa wananchi na kwamba ana imani mradi huo utatekelezwa kwa mafanikio na kuchangia upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Tunduma na Vwawa-Mlowo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, alisema mradi huo umefika wakati muafaka kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na ukuaji wa kasi wa miji unaoongeza shinikizo katika rasilimali za maji.

Alisema utekelezaji wa mradi huo utaimarisha usimamizi wa rasilimali za maji unaozingatia athari za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa uhakika katika maeneo husika.

Mhandisi Mwajuma alibainisha kuwa Wizara ya Maji itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi, uwazi na kwa wakati, kwa kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali ili kuhakikisha unaleta manufaa ya kudumu kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment