MAJAJI WAJENGEWA UWEZO KATIKA USIKILIZAJI WA KESI ZA UBUNIFU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 12, 2026

MAJAJI WAJENGEWA UWEZO KATIKA USIKILIZAJI WA KESI ZA UBUNIFU

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Majaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu masuala ya haki miliki, hatua inayolenga kuwajengea uwezo katika usikilizaji na utoaji wa maamuzi yanayohusu ubunifu, kazi za wasanii, wabunifu pamoja na wavumbuzi nchini.

Mafunzo hayo yamefanyika leo Mei 11, 2026 jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano wa wadau wa sheria na taasisi zinazoshughulikia haki miliki, yakiwahusisha majaji pamoja na maafisa wa mahakama, hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na ongezeko la migogoro inayohusu haki miliki.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Jaji Kiongozi, Jaji wa Mahakama Kuu, Iman Aboud amesema ongezeko la mashauri ya haki miliki nchini linahitaji watendaji wa mahakama kuwa na uelewa mpana wa sheria hizo ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati na kwa usahihi.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uelewa wa sheria za miliki ubunifu pamoja na kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa mashauri yanayohusu sekta hiyo.

“Maendeleo ya nchi yoyote yanategemea ubunifu. Hata hivyo, wamiliki wa ubunifu huo wamekuwa wakikumbana na changamoto za kisheria zinazofikishwa mahakamani. Ni muhimu kwa sisi tunaosikiliza na kutafsiri sheria kuelewa kwa kina masuala haya ili kuhakikisha haki zinatendeka ipasavyo,” amesema Jaji Aboud.

Aidha, amesema maamuzi ya mahakama yana athari pana ndani na nje ya nchi, kwani hutumika kama rejea katika utoaji wa haki kwenye maeneo mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na uelewa wa kina kuhusu sheria za haki miliki.

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, Dkt. Cleoface Morris amesema mashauri mengi yanayowasilishwa mahakamani yanahitaji tafsiri sahihi ya sheria ili kuimarisha usimamizi wa haki za miliki ubunifu.

“Mafunzo haya yatatusaidia kuwa na uwiano katika utoaji wa maamuzi ndani ya Mahakama Kuu, hasa kwa kuzingatia kuwa mashauri mengi yanafanana kimuktadha,” amesema Dkt. Morris.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa amesema mahakama ina mchango mkubwa katika utekelezaji wa sheria zinazolinda walaji pamoja na kusimamia haki za miliki.

Amesema moja ya majukumu ya FCC ni kusajili nembo na alama za bidhaa ili kusaidia kutambua bidhaa halisi zilizopo sokoni na kubaini bidhaa bandia kwa lengo la kumlinda mlaji.

Bi. Ngasongwa amesema mafunzo hayo yatawasaidia majaji kuwa na uelewa mpana wa masuala ya kisheria pamoja na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ya sheria ili kuhakikisha upatikanaji wa tafsiri sahihi za kisheria katika mashauri ya miliki ubunifu.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi endelevu za taasisi hiyo kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wa sheria kuhusu umuhimu wa miliki ubunifu nchini.

Amesema maamuzi ya majaji yana mchango mkubwa katika kulinda maslahi ya taifa katika sekta ya ubunifu na kuongeza kuwa tayari zipo hukumu mbalimbali ambazo zimekuwa msaada mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya BRELA.

“Tumeleta wataalamu wa miliki ubunifu ili kujenga uelewa wa pamoja. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo kila ubunifu unalindwa kisheria kwa kuwa ni chanzo muhimu cha kipato kwa mtu binafsi na taifa kwa ujumla,” amesema Bw. Nyaisa.

BRELA imekuwa ikiendesha mafunzo ya miliki ubunifu kwa majaji pamoja na wadau mbalimbali wa sheria nchini kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kujenga uelewa mpana kuhusu haki miliki katika jamii.

No comments:

Post a Comment