DKT. MWIGULU AAGIZA WALIOIBA MILIONI 500 MANYONI KUKAMATWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 30, 2026

DKT. MWIGULU AAGIZA WALIOIBA MILIONI 500 MANYONI KUKAMATWA


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza watumishi waliohusishwa na ubadhirifu wa zaidi ya shilingi milioni 500 katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni watafutwe popote walipo, wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria na kinidhamu huku fedha hizo zikirejeshwa serikalini.

"Wamechota fedha za wananchi. Watafutwe hata ambao walishahamishwa, popote walipo wakamatwe, wawekwe ndani na fedha za Serikali zirudi. Hii si fedha ya mtu binafsi, ni fedha ya wananchi," alisema Dkt. Mwigulu.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo Jumamosi Mei 30, 2026 alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Manyoni katika Viwanja vya Tambukareli mkoani Singida akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.

Alisema taarifa alizopokea zinaonesha kuwa jumla ya zaidi ya shilingi milioni 501 zilichotwa kutoka akaunti mbalimbali za halmashauri ikiwemo Akaunti ya Maendeleo (zaidi ya shilingi milioni 213), Akaunti ya Amana (zaidi ya shilingi milioni 259) na Akaunti ya Mapato ya Ndani (zaidi ya shilingi milioni 42), jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa na Serikali.

Waziri Mkuu aliwataja watumishi wanaodaiwa kuhusika katika ubadhirifu huo kuwa ni aliyekuwa Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo Mwakapala, ambaye kwa sasa amehamishiwa mkoani Songwe, Mhasibu wa Mapato Edward Kilungu na Eliamini Maliki.

Aidha, alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida (RPC) kuhakikisha watumishi hao wanatafutwa, wanakamatwa na kuwekwa mahabusu hadi fedha za Serikali zitakapopatikana.

"Mweka Hazina Mwakapala arudishwe, Edward Kilungu na Eliamini Maliki watafutwe. Wakamatwe, wawekwe ndani na wasitoke mpaka fedha ya Serikali irudi," alisema Dkt. Mwigulu.

Aidha, Waziri Mkuu alimuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuhakikisha watumishi wote waliohusika wanasimamishwa kazi mara moja huku taratibu za kinidhamu na kisheria zikiendelea.

"Barua za kuwasimamisha kazi zitoke leo leo na hatua zinazostahili za kiutumishi zifanyike haraka. Wasitoke mpaka fedha za wananchi zirudi," alisema.

Sambamba na hilo, Dkt. Mwigulu alikemea vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na matumizi mabaya ya madaraka, akieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita haitamvumilia mtu yeyote atakayehujumu rasilimali za wananchi.

"Ninachukia uvivu, uzembe, wizi na kuonewa kwa wanyonge. Nitawashikisha adabu wezi, walaghai na wote wanaotumia nafasi zao kuwaumiza wananchi," alisema.

Aidha, alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida pamoja na vyombo vya Serikali kwa kugundua na kuanza kuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alikemea tabia ya baadhi ya viongozi kutumia muda mwingi kufikiria uchaguzi na vyeo badala ya kutatua changamoto za wananchi, akisisitiza kuwa Watanzania wanahitaji maendeleo na huduma bora zaidi kuliko siasa za makundi.

"Watanzania wana kiu ya maendeleo. Kiu waliyonayo si ya kugawana madaraka, bali ni maendeleo na kuondoka kwa kero zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku," alisema.

Aliongeza kuwa viongozi wanapaswa kutumia nafasi walizopewa kutatua matatizo ya wananchi badala ya kutumia muda mwingi kufuatilia nafasi nyingine za uongozi.

"Kila mmoja afanye kazi katika nafasi aliyopewa. Watanzania wana shida nyingi zinazohitaji ufumbuzi na si siasa za makundi au mbio za madaraka," alisema.

Pia, Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kusimamia haki za wananchi, kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma na kuhakikisha fedha za maendeleo zinafika na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza hatua mbalimbali za kuboresha maisha ya wananchi ikiwemo kutoa elimu bila ada kwa Kidato cha Tano na Sita, Programu ya Samia Scholarship na kuondoa riba kwa mikopo ya elimu ya juu kwa wahitimu ambao hawajapata ajira.

Aidha, alieleza kuwa Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), miradi ya maji, afya, barabara na usambazaji wa umeme vijijini ili kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

Waziri Mkuu aliwahakikishia wananchi wa Manyoni na Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha matunda ya maendeleo yanawafikia wananchi wote.

"Niwahakikishie Watanzania kwamba yote yaliyomo kwenye Ilani na ahadi za Mheshimiwa Rais yataendelea kutekelezwa kwa manufaa ya wananchi," alisema.

No comments:

Post a Comment