Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameagiza Menejimenti ya Kiwanda cha Kuzalisha Bidhaa za Kibaolojia Tanzania (TBPL) kinachomilikiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kuongeza uzalishaji na kuimarisha mikakati ya masoko ili kunufaika na mahitaji makubwa yaliyopo sokoni, kuhakikisha kiwanda kinaendelea kujiendesha kwa ufanisi wa kibiashara
Vilvile amezitaka Taasisi zote hususani TFC, TARI, TFRA na TPHPA zilizoingia makubaliano na TBPL kuhakikisha yanatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yenye manufaa kwa wakulima, sekta ya viwanda na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Ametoa maagizo hayo Mei 30, 2026 katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano iliyofanyika katika Kiwanda cha TBPL kilichopo Kibaha mkoani Pwani, kwa lengo la kuimarisha uzalishaji, usambazaji na matumizi ya mbolea hai nchini.
Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano uliowekwa kati ya TBPL, na Taasisi hizo ni hatua muhimu katika kuimarisha minyororo ya thamani ya Mazao ya kilimo na viwanda pamoja na kukuza matumizi ya teknolojia na ubunifu.
Aidha, Waziri Kapinga amesema uzalishaji wa mbolea hai nchini utapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza pembejeo hizo kutoka nje ya nchi huku ukiwawezesha wakulima kupata bidhaa bora kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Waziri Kapinga pia ameeleza kuwa matumizi ya mbolea hai kupitia TBPL ni hatua muhimu katika kuongeza tija ya kilimo, kuchochea ukuaji wa viwanda vinavyotegemea malighafi za ndani na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa mbolea hai katika ukanda wa Afrika Mashariki..




















No comments:
Post a Comment