
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Janeth Mawahanga ameisifu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa ya uboreshaji wa miundombinu yanayoendelea kuonekana katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati wa kuchangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 leo Alhamisi Mei 21, 2026, Mawahanga amesema Dar es Salaam imeendelea kupata sura mpya kutokana na uwekezaji mkubwa wa barabara na miundombinu mingine muhimu inayotekelezwa na serikali.
Amesema maendeleo hayo yamesaidia kupunguza changamoto ya foleni iliyokuwa ikiwasumbua wananchi kwa muda mrefu, huku barabara za ndani zilizoboreshwa zikichochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya jiji.
Mawahanga amesema uwekaji wa taa za barabarani umeongeza usalama na kutoa fursa kwa wananchi kufanya biashara hadi usiku, jambo ambalo limeongeza mzunguko wa fedha na kuimarisha uchumi wa wakazi wa Dar es Salaam.
Aidha, alimpongeza Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na wataalamu wa wizara hiyo kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika kuhakikisha miundombinu ya Dar es Salaam inaendelea kuimarika.
“Dar es Salaam ndiyo kitovu cha biashara nchini, hivyo maboresho haya ya miundombinu yanaongeza hadhi ya mkoa wetu na kurahisisha maisha ya wananchi,” alisema Mawahanga.
Mbunge huyo amesema kasi ya maendeleo ya miundombinu imeifanya Dar es Salaam kubadilika kwa kiwango kikubwa, huku maeneo mengi yakiongezeka thamani kutokana na wananchi kuhamia pembezoni mwa jiji kujenga makazi mapya kufuatia kuboreshwa kwa miundombinu.
Pia ameitaka serikali kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa barabara za ndani katika mkoa huo ili kupunguza msongamano katika barabara kuu zinazotumiwa na maelfu ya wananchi wanaoingia na kutoka katikati ya jiji kila siku.
Amesema kutokana na Dar es Salaam kuwa mkoa unaoingiza pato kubwa la taifa na wenye ongezeko kubwa la watu kila siku, ipo haja ya kuendelea kuboresha miundombinu yake ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi na idadi ya watu.

No comments:
Post a Comment