MIUNDOMBINU YA UTALII YAFUNGUA FURSA YA AJIRA NA BIASHARA NCHINI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 15, 2026

MIUNDOMBINU YA UTALII YAFUNGUA FURSA YA AJIRA NA BIASHARA NCHINI.


Na Mwandishi Wetu , Dodoma


Serikali imeendelea kuwekeza na kuimarisha miundombinu katika sekta ya utalii, kwa kujenga viwanja vya ndege, Barabara, na maeneo ya malazi ili kukuza mchango wa sekta hiyo katika Uchumi wa Taifa.

Hayo yamebainishwa leo Mei 15, 2026 Bungeni Dodoma na Waziri wa Maliasili na utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Pamoja na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.


Dkt. Kijaji amesema, Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mhifadhi na Muongoza Watalii namba moja nchini imekamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege vitatu (3) katika Hifadhi za Taifa za Nyerere (1) na Ruaha (2) pamoja na kukarabati viwanja vya ndege nane (8) katika Hifadhi za Taifa za Mikumi (1), Ruaha (2), Nyerere (2) na Serengeti (3).


“Jumla ya kilomita 3,757.92 za barabara na kilomita 523.14 za njia za watembea kwa miguu zimejengwa na kukarabatiwa katika maeneo yaliyohifadhiwa ili kurahisisha ufikaji kwenye vivutio vya utalii”. Alisema Dkt. Kijaji.

Ameongeza kuwa uwekezaji huo umechechemua sekta ya utalii kwa kurahisisha ufikiwaji wa vivutio vya utalii, kuboresha uzoefu wa wageni na kufungua fursa za ajira na biashara kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi.

“Vilevile, umechangia ongezeko la mapato ya Serikali na ukuaji wa sekta kwa ujumla. Mathalan, katika Ukanda wa Kusini, maboresho haya yamewezesha ongezeko la watalii kutoka 197,402 hadi kufikia 205,520 na mapato kuongezeka kutoka Shilingi bilioni 24.6 hadi bilioni 27.7 katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026”. Alifafanua Dkt. Kijaji

 Aidha, ameongeza kuwa, mafanikio hayo yana akisi dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha miundombinu ya utalii ili kuongeza ushindani wa Tanzania kimataifa, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.

No comments:

Post a Comment