
Mbunge wa Gairo, Mhe. Ahmed Shabiby, amesema Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) imekuwa ikitoa ushirikiano wa karibu kila inapohitajika katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye Vipimo sahihi, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha usimamizi wa vipimo na kulinda maslahi ya wananchi pamoja na wafanyabiashara nchini.
Amempongeza Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA ndugu Alban Kihulla, kwa uongozi wake wenye weledi na ushirikiano mzuri katika kusimamia majukumu ya taasisi hiyo.
Akichangia bungeni wakati wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Shabiby alisema WMA imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kushirikiana kikamilifu na wadau mbalimbali katika kuhakikisha usimamizi wa vipimo unakuwa imara nchini.
Hata hivyo, ameitaka WMA kuongeza umakini katika kusimamia usahihi wa Vipimo kwenye bidhaa za chuma kama nondo zinazozalishwa na baadhi ya viwanda nchini, akibainisha kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya bidhaa hizo kutokidhi vipimo vinavyotakiwa.
Amesema baadhi ya viwanda vinavyoendeshwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi vinaendelea kuzalisha nondo zisizo na vipimo sahihi, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa majengo na maisha ya wananchi.
“Tusibaki kwenye kutoa faini pekee. Viwanda vinavyotengeneza nondo zisizokidhi vipimo vinapaswa kuchukuliwa hatua kali, ikiwemo kufungiwa, ili kulinda usalama wa wananchi na ubora wa ujenzi nchini,” amesema Shabiby.
Ameongeza kuwa usimamizi madhubuti wa Vipimo vya bidhaa za ujenzi ni msingi muhimu wa kukuza sekta ya viwanda na kulinda usalama wa miundombinu nchini.
Wakala wa Vipimo inaendelea kusimamia matumizi sahihi ya Vipimo nchini kama Sheria ya Vipimo Sura 340 inavyoelekeza ili kuhakikisha mwananchi anapata bidhaa sahihi kulingana na kiasi cha fedha anachotoa.

No comments:
Post a Comment