TANZANIA YAIMARISHA UWEZESHAJI BIASHARA KUPITIA WTO NA UNCTAD - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 22, 2026

TANZANIA YAIMARISHA UWEZESHAJI BIASHARA KUPITIA WTO NA UNCTAD



Na Okuly Julius,OKULY BLOG,DODOMA


SERIKALI imeendelea kuimarisha mazingira ya biashara nchini kupitia utekelezaji wa Mkataba wa Uwezeshaji Biashara wa Shirika la Biashara Duniani (WTO-TFA) pamoja na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya biashara.

Hayo yameelezwa bungeni na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Waziri Kapinga amesema Wizara kupitia Kamati ya Kitaifa ya Uwezeshaji Biashara (NCTF) inaendelea kutekeleza Mkataba wa Uwezeshaji Biashara wa Shirika la Biashara Duniani sambamba na kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kutafuta ufadhili wa miradi ya utekelezaji wa mkataba huo.

Amesema Kamati hiyo pia inaendelea kufanya mapitio ya Mpango Mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli zake za miaka mitano kupitia zoezi la kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya biashara.

Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amesema Kamati ya Kitaifa ya Uwezeshaji Biashara imeendelea kutatua changamoto za wafanyabiashara kupitia kliniki maalum za biashara hususan katika mpaka wa Tunduma.

Kupitia kliniki hizo, wafanyabiashara wamepatiwa elimu kuhusu taratibu za kuvuka mipaka, matumizi ya mfumo uliorahisishwa kwa wafanyabiashara wadogo, uondoshaji na upitishaji wa mizigo pamoja na fursa za biashara ya kikanda.

Amesema jumla ya wafanyabiashara 72 wamenufaika na mafunzo hayo yaliyolenga kurahisisha shughuli za biashara na kuongeza uelewa wa taratibu za biashara za kikanda na kimataifa.

Waziri Kapinga pia amesema Tanzania ilishiriki Mkutano wa 16 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) uliofanyika Oktoba 2025 mjini Geneva, Switzerland ukiwakutanisha wakuu wa nchi, mawaziri wa biashara na uchumi pamoja na wataalam wa biashara duniani.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mkutano huo ulijadili masuala ya usalama wa bidhaa za watumiaji na kuweka mapendekezo ya kuimarisha usalama wa bidhaa kupitia mageuzi ya kitaifa pamoja na ushirikiano wa kimataifa.

Vipaumbele vilivyokubaliwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya udhibiti, kuboresha tathmini ya hatari na ukusanyaji wa taarifa, kuimarisha mifumo ya kubadilishana taarifa za biashara za kuvuka mipaka pamoja na kuzingatia mahitaji ya nchi zinazoendelea.

Aidha, Waziri Kapinga amesema Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika uwasilishaji wa taarifa za biashara kwa Shirika la Biashara Duniani kupitia mfumo wa e-ping.

Amesema hadi Aprili 2026, Tanzania ilikuwa imewasilisha jumla ya taarifa 506 zinazohusu biashara, ikiwemo masuala ya viwango, afya ya mimea na wanyama, usalama wa chakula, ruzuku za biashara pamoja na ushuru wa mipakani.

Waziri huyo amesema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2025, Tanzania imefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi 10 bora kati ya nchi 166 wanachama wa Shirika la Biashara Duniani katika uwasilishaji wa taarifa za Vikwazo vya Biashara vya Kiufundi (TBT).

Amesema mafanikio hayo yanaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazozingatia uwazi na ufanisi katika biashara ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment