-Arusha
Wahasibu na wachumi wametakiwa kujijengea nidhamu ya kitaaluma kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa ili kujiepusha na vitendo vya udukuzi wa mifumo ya kielektroniki na kulinda taarifa za Serikali.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, CPA Idfonce Masoud, baada ya mawasilisho kuhusu faida za Mfumo Jumuishi wa Kodi za Ndani (IDRAS), mifumo mipya ya ukusanyaji wa mapato na usalama wa mifumo kwenye kikao kazi cha wahasibu na wachumi wa Tume ya Madini kilichofanyika jijini Arusha.
CPA Masoud amesema usiri wa taarifa mahala pa kazi ni jambo muhimu katika taaluma ya uhasibu na uchumi, huku akisisitiza kuwa maadili na uwajibikaji vinapaswa kupewa kipaumbele ili kuongeza ufanisi wa kazi na kulinda taswira ya taasisi.
“Maadili ni muhimu katika maeneo ya kazi; bila kuwa na maadili hata kazi zetu hazitaheshimiwa na kuharibu taswira ya taasisi,” amesema.
Kwa upande wake, Meneja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Jastin Chankani, amesema wahasibu, wachumi na watumishi wengine wanapaswa kutumia mifumo ya kielektroniki kwa usalama ili kulinda taarifa za Serikali na rasilimali za umma.
Amesema wahasibu ni kundi muhimu kwa kuwa hushughulikia taarifa za mapato na matumizi ya Tume, hivyo wanapaswa kuwa makini dhidi ya wadukuzi wenye nia mbaya.
“Ulinzi wa taarifa ni muhimu ili kuhifadhi usalama wa mitandao ya ofisi na kuzuia uvunjaji wa faragha pamoja na matumizi mabaya ya rasilimali za umma,” amesema Chankani.
Naye Afisa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania, Deogratius Mrosso, ameeleza kuwa Mfumo Jumuishi wa Kodi za Ndani (IDRAS) utawezesha utoaji wa huduma za kodi kwa saa 24 kila siku, kuhifadhi kumbukumbu za kodi, kutoa risiti za kielektroniki bila kutumia mashine, kuthibitisha nyaraka za kodi na kuonesha taarifa za kikodi za waajiriwa.
Amesema mfumo huo utaongeza uwazi, ufanisi na urahisi katika utoaji wa huduma za kodi nchini.
Aidha, Meneja wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Frank Mbele, amewataka wahasibu na wachumi kufanya kazi kwa bidii na kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Tume pamoja na viashiria vya utendaji ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Washiriki wa kikao hicho wamehimizwa kuendelea kuimarisha usalama wa mifumo ya kielektroniki na kushirikiana katika kuboresha miundombinu ya teknolojia kwa lengo la kuongeza uwazi, ulinzi wa taarifa na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kwa manufaa ya umma.









No comments:
Post a Comment