WAZIRI MKUU APONGEZA KILIMO CHA KOROSHO MANYONI, AHIMIZA UONGEZAJI THAMANI WA MAZAO KUPITIA VIWANDA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, May 30, 2026

WAZIRI MKUU APONGEZA KILIMO CHA KOROSHO MANYONI, AHIMIZA UONGEZAJI THAMANI WA MAZAO KUPITIA VIWANDA


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza uchumi wa viwanda na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, huku akiwataka vijana, sekta binafsi na wawekezaji kutumia fursa zilizopo kuanzisha viwanda vya kuchakata korosho na mazao mengine ya kilimo.

“Serikali haipaswi kufanya jukumu hilo peke yake la kujenga viwanda. Lakini kwa kuwa zao hili halikuwa zao la asili lililozoeleka kwa Mkoa wa Singida, ni lazima hatua za aina hii ziweze kufanyika. Baada ya hapo vijana na sekta binafsi wachukue jukumu hilo la kutengeneza viwanda vya kutosha vya kubangua korosho zinazozalishwa hapa Mkoa wa Singida na pengine hata mikoa mingine,” alisema Dkt. Mwigulu.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo Jumamosi Mei 30, 2026 alipokagua Mradi wa Mnyororo wa Thamani wa Korosho kupitia Kiwanda Darasa cha Kubangua Korosho (KIDAKUKO) cha CAMARTEC kilichopo Masigati wilayani Manyoni, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Singida.

Waziri Mkuu aliwapongeza wananchi wa Manyoni kwa kuendelea kuimarisha kilimo cha korosho na kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoanzisha kwa mafanikio zao hilo katika Mkoa wa Singida.

“Niwapongeze ndugu zetu wa Manyoni kwa kuanza kuwa wa kwanza kulima zao hili la korosho kwa Mkoa wa Singida. Hongereni sana, mmetupandisha chati wote,” alisema.

Alisema zao la korosho ni miongoni mwa mazao mbadala yenye umuhimu mkubwa katika kuimarisha uchumi wa wananchi na taifa kutokana na mabadiliko yanayoendelea kujitokeza katika masoko ya mazao mbalimbali duniani.

“Kuna mazao ambayo zamani yalikuwa yanafanya vizuri sana duniani, lakini yanaendelea kupata changamoto. Kadri tunapopata changamoto katika zao moja, lazima tuwe na mazao mbadala mengi. Sasa kwa Manyoni imeanza vizuri hili zao la korosho,” alisema.

Aidha, Dkt. Mwigulu alisema Kiwanda Darasa hicho kinaendana na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea uzalishaji, viwanda, teknolojia na uwekezaji wa sekta binafsi.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC), Mhandisi Godfrey Mwinama, alimweleza Waziri Mkuu kuwa Kiwanda Darasa cha Kubangua Korosho (KIDAKUKO) cha Masigati kilijengwa kwa gharama ya shilingi milioni 637.5 na kilizinduliwa rasmi Septemba 30, 2025.

Mhandisi Mwinama alisema kiwanda hicho ni miongoni mwa jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha matokeo ya tafiti na ubunifu wa ndani yanawanufaisha wananchi kupitia uzalishaji, uchakataji na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Alisema kiwanda hicho kilianzishwa kwa lengo la kutoa mafunzo ya ubanguaji na uchakataji wa korosho kwa vijana, wanawake na wawekezaji, huku kikiwa na uwezo wa kufundisha watu 50 kwa wakati mmoja.

Aidha, alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kubangua kati ya tani 1.36 hadi tani 2.72 za korosho kwa siku kulingana na kiwango cha uzalishaji na uzoefu wa wabanguaji.

“Teknolojia nyingi zinazotumika katika kiwanda hiki zimeundwa hapa nchini. Zipo mashine za kubangua korosho, makaushio, vifaa vya uchambuzi wa korosho na mifumo mingine ya uchakataji iliyobuniwa na wataalamu wa CAMARTEC,” alisema Mhandisi Mwinama.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Bodi ya Korosho Tanzania Ray Mtangi alisema Serikali imeendelea kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la korosho kupitia huduma za ugani, pembejeo za ruzuku, ushirika wa wakulima, maghala ya kuhifadhi mazao na mifumo ya kisasa ya uuzaji wa korosho.

Taarifa ya CAMARTEC ilieleza kuwa endapo korosho zote zinazozalishwa nchini zitachakatwa hapa nchini, zaidi ya ajira 36,458 zinaweza kuzalishwa sambamba na kuongeza mapato ya wananchi na thamani ya bidhaa zitokanazo na zao hilo.

No comments:

Post a Comment