WIZARA YA MAJI YAOMBA KUIDHINISHIWA TRILIONI 1.12 KUTEKELEZA MIRADI YA MAJI 2026/27 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 5, 2026

WIZARA YA MAJI YAOMBA KUIDHINISHIWA TRILIONI 1.12 KUTEKELEZA MIRADI YA MAJI 2026/27



Okuly Julius ,OKULY BLOG,DODOMA


Serikali imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 1.12 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Maji katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za majisafi na usafi wa mazingira nchini.


Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema kiasi hicho kinajumuisha Shilingi 1,120,194,614,000, ambapo Shilingi bilioni 80.65 ni kwa matumizi ya kawaida na Shilingi trilioni 1.039 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.


Aweso amesema kati ya fedha za matumizi ya kawaida, Shilingi bilioni 16.27 zitatumika kwa matumizi mengineyo (OC), huku Shilingi bilioni 64.37 zikielekezwa katika mishahara ya watumishi wa Wizara, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mfuko wa Taifa wa Maji pamoja na Chuo cha Maji.


Kwa upande wa fedha za maendeleo, amesema Shilingi bilioni 401.2 ni fedha za ndani, huku Shilingi bilioni 638.33 zikiwa ni fedha kutoka vyanzo vya nje, zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini.


Amesisitiza kuwa fedha hizo zitawezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji, kuimarisha miundombinu ya usambazaji majisafi, pamoja na kuboresha huduma za usafi wa mazingira ili kukidhi mahitaji ya wananchi.


Aweso ameliomba Bunge kuidhinisha bajeti hiyo ili kuwezesha Wizara kuendelea na juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama unafikiwa kwa kiwango kikubwa zaidi nchini.

No comments:

Post a Comment