
Na Okuly Julius, OKULY BLOG , DODOMA
Bunge limeidhinisha jumla ya Sh. bilioni 108.024 kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele saba vya kimkakati vinavyolenga kujenga jamii imara, jumuishi na yenye maendeleo endelevu nchini.
Kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 50.138 zitatumika kwa matumizi ya kawaida, huku Sh. bilioni 57.886 zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Dkt Dorothy Gwajima , amesema katika mwaka 2026/27 wizara itajikita katika maeneo yenye matokeo chanya kwa taifa, uwezo wa kuleta mageuzi na mchango mkubwa katika maendeleo ya wananchi.
Amesema kipaumbele cha kwanza ni kujenga mtaji watu wa taifa na kizazi cha Tanzania ya mwaka 2050 kitakachozingatia maadili, uzalendo, haki, usawa, ustawi na maendeleo jumuishi.
Kipaumbele cha pili ni kuimarisha huduma za ustawi, malezi na makuzi ya watoto, ulinzi wa kijamii na uthabiti wa taifa ili kuendeleza jamii yenye mshikamano, ustahimilivu na utu wa kibinadamu.
Aidha, wizara itaimarisha mifumo ya uwezeshaji wanawake, kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili wa kijinsia ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Katika eneo la uchumi, wizara imepanga kufanya mageuzi ya uchumi wa makundi maalum na sekta isiyo rasmi kwa kuyabadilisha kutoka uchumi wa kujikimu kwenda uchumi rasmi wa kibiashara wenye tija, ushindani na mchango mkubwa katika pato la taifa.
Pia, wizara itapanua matumizi ya teknolojia za kidijitali na takwimu katika utoaji wa huduma za kijamii ili kurahisisha utendaji na kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kitakwimu.
Vipaumbele vingine ni kujenga jamii yenye amani, uwajibikaji na mshikamano pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi, taasisi za dini na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa Waziri Gwajima, utekelezaji wa vipaumbele hivyo unalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa na jamii yenye ustawi, inayowezesha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kuelekea utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.





No comments:
Post a Comment