
Kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Yemen, Mhe. Abedrabbo Mansour Hadi, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Abdallah Kilima, tarehe 4 Juni 2026 amesaini kitabu cha maombolezo katika Ubalozi wa Jamhuri ya Yemen jijini Dar Es Salaam.
Alisaini kitabu hicho kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuwasilisha salamu za pole kutoka kwa Watanzania wote kwenda kwa familia, serikali na wananchi wa Jamhuri ya Yemen.
Akizungumza na Kaimu Balozi wa Jamhuri ya Yemen nchini, Bw. Ahmed Saleh Al Omry, Balozi Kilima alisema marehemu Hadi atakumbukwa kwa mchango wake katika kuhimiza amani na utulivu. Alieleza kuwa msiba huo ni pigo kubwa kwa wote wanaothamini amani duniani.
Balozi Kilima alisisitiza kuwa Tanzania inaungana na wananchi wa Jamhuri ya Yemen katika kipindi hiki cha majonzi kutokana na uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizo mbili.
Aidha, alisema Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Yemen ili kudumisha uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia uliopo. Marehemu Hadi alifariki tarehe 28 Mei 2026 mjini Riyadh, Saudi Arabia, akiwa na umri wa miaka 80.




No comments:
Post a Comment