MWENGE WA UHURU WAPONGEZA MRADI WA MAJI NALA, WANANCHI 5,188 KUNUFAIKA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 1, 2026

MWENGE WA UHURU WAPONGEZA MRADI WA MAJI NALA, WANANCHI 5,188 KUNUFAIKA


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amepongeza utekelezaji wa mradi wa maji safi katika Kata ya Nala jijini Dodoma, akieleza kuwa mradi huo umeleta mapinduzi makubwa ya huduma ya maji kwa wananchi pamoja na kusaidia uwekezaji wa viwanda.


Akizungumza leo Juni 1, 2026 wakati wa uzinduzi na ukaguzi wa mradi huo uliofanywa na Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mwang’onda alisema Mwenge wa Uhuru umeridhishwa na ubora wa mradi huo uliotekelezwa na Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Dodoma (DUWASA).


“Mwenge wa Uhuru umefika katika mradi huu, umepokea taarifa na kuukagua. Baada ya ukaguzi tumeridhishwa kuona kuwa mradi umekamilika vizuri na DUWASA wamefanya kazi kubwa sana,” alisema Mwang’onda.


Alieleza kuwa mradi huo umeletwa mahsusi kwa ajili ya wananchi wa Nala lakini pia kusaidia shughuli za uwekezaji wa viwanda, ikiwemo kiwanda kikubwa cha mbolea cha Nala Intracom kinachotegemea huduma ya maji katika uzalishaji wake.


“Maji haya yanawahudumia wananchi lakini pia yanapelekwa viwandani. Hili ni jambo kubwa kwa maendeleo ya eneo hili,” alisema.


Aidha alisema eneo la Nala lina vyanzo vyenye uwezo mkubwa wa uzalishaji maji ambapo kisima kimoja kina uwezo wa kujaza tanki la lita 200,000 ndani ya saa tatu pekee.


Mwang’onda alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha zilizowezesha utekelezaji wa mradi huo, akisema hatua hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Nala waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu.


Alisema Rais Samia anaendelea kuwaomba Watanzania kudumisha amani na utulivu huku serikali ikiendelea kuwaletea maendeleo na huduma muhimu za kijamii.


“Mwenge wa Uhuru umefurahishwa sana na mradi huu. Tunaomba huduma ya maji iendelee kusambazwa ili wananchi wengi zaidi waendelee kupata maji safi na salama,” alisema.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nala, Leonard Alexander, alisema wananchi wa eneo hilo wamepokea kwa furaha kubwa ujio wa mradi huo kwani umeondoa kwa kiasi kikubwa adha ya upatikanaji wa maji.


Alisema kabla ya utekelezaji wa mradi huo wananchi walilazimika kutembea umbali wa kilomita mbili hadi tano kutafuta maji, licha ya eneo hilo kuwa karibu na Jiji la Dodoma.


“Kwa sasa zaidi ya wananchi 500 hadi 1,000 wameunganishiwa huduma ya maji majumbani mwao. Wananchi wanafungua maji na kuyatumia kwa urahisi tofauti na zamani,” alisema.


Aliongeza kuwa mradi huo umeongeza fursa za ajira katika kiwanda cha mbolea kutokana na upatikanaji wa maji ya uhakika, huku pia ukileta utulivu katika familia nyingi.


“Maji yameleta amani hata kwenye ndoa zetu kwa sababu huduma imekuwa rahisi kupatikana. Tunamshukuru sana Rais Samia, viongozi wa Mwenge wa Uhuru, uongozi wa wilaya pamoja na DUWASA kwa kuwaletea wananchi tabasamu,” alisema.


Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Benard Rugaui, akisoma risala ya mradi huo alisema lengo kuu la mradi ni kuboresha huduma ya maji na kuongeza uzalishaji kutoka lita milioni 88.94 hadi kufikia lita milioni 91.2 kwa siku, sawa na ongezeko la asilimia 2.5.


Alisema mradi huo umegharimu jumla ya Sh bilioni 1.604, fedha zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Kwa mujibu wa Rugaui, utekelezaji wa mradi ulianza Julai 1, 2024 na kukamilika Mei 31, 2025 kwa muda wa takribani miezi 10.


Alisema mradi huo unahudumia wakazi 5,188 wa maeneo ya Nala Center, Segu Juu na Chihoni pamoja na kiwanda cha mbolea cha Nala Intracom.


Aidha alisema kukamilika kwa mradi huo kumeongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika Kata ya Nala kutoka asilimia 9 hadi asilimia 60 kwa sasa.


Rugaui alibainisha kuwa maeneo yanayohudumiwa na DUWASA katika Wilaya ya Dodoma yana jumla ya wakazi 851,633 wenye mahitaji ya maji ya lita milioni 159.9 kwa siku.


Alitaja vyanzo vikuu vya maji kuwa ni Bonde la Mzakwe lenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 61.5 kwa siku, Nzuguni lita milioni 10, Iyumbu lita milioni 7.32 pamoja na visima vya pembezoni vinavyozalisha lita milioni 6.2 kwa siku.


Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kata ya Nala walisema mradi huo umekuwa mkombozi mkubwa kwao kwani hapo awali walikuwa wakitumia muda mwingi na gharama kubwa kutafuta maji, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa katika maisha yao ya kila siku.


Walisema kwa sasa huduma ya maji imewafikia karibu na makazi yao jambo ambalo limeongeza faraja na kuboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa.





No comments:

Post a Comment