SERIKALI KUTOA FEDHA ZA DHARURA KUKARABATI BARABARA ZILIZOHARIBIWA NA MVUA BUKOBA MJINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 2, 2026

SERIKALI KUTOA FEDHA ZA DHARURA KUKARABATI BARABARA ZILIZOHARIBIWA NA MVUA BUKOBA MJINI


Na Gideon Gregory  - Dodoma


Serikali imesema imeanza kuchukua hatua za dharura za kukarabati barabara zilizoharibiwa na mvua katika Jimbo la Bukoba Mjini ili kurejesha shughuli za usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo ya uzalishaji.


Kauli hiyo imetolewa leo Juni 02,2026 Bungeni Jijini Dodoma Naibu Waziri w Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Dkt. Festo Dugange wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Bukoba Mjini Mha. Johnston Mutasigwa, ambaye alitaka kujua kama Serikali iko tayari kutoa fedha za dharura kwa ajili ya matengenezo ya barabara muhimu zilizoharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.


Akiuliza swali hilo bungeni, Mbunge huyo amesema kuwa mvua hizo zimesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara katika jimbo hilo, hususan kwenye barabara zinazounganisha maeneo ya uzalishaji wa uvuvi na shughuli nyingine za kiuchumi. Akitaja barabara za Kahororo–Kifungwa, Pepsi–Nyamkazi kwenye kiwamda cha Samako na Makongo–Ntoro kuwa miongoni mwa zilizoathirika zaidi.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri amesema Serikali imefanya tathmini ya barabara zote zilizoathiriwa na mvua katika Manispaa ya Bukoba na tayari imeanza kutenga fedha kupitia bajeti ya dharura ya Mkoa wa Kagera kwa ajili ya matengenezo yake.


Aidha, amempongeza Mbunge huyo kwa kufuatilia kwa karibu changamoto za miundombinu katika jimbo lake na kubainisha kuwa Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa maeneo yanayonufaika na miradi ya TARURA inayolenga kuboresha miundombinu ya barabara.


Naibu Waziri pia amewataka Meneja wa TARURA Wilaya ya Bukoba pamoja na Meneja wa TARURA Mkoa wa Kagera kuhakikisha taratibu za manunuzi zinakamilika kwa wakati ili wakandarasi waanze haraka kazi za ukarabati wa barabara hizo.


Amesema kukamilika kwa matengenezo hayo kutasaidia kurejesha huduma za usafiri na usafirishaji pamoja na kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Bukoba Mjini na maeneo ya jirani.

No comments:

Post a Comment