SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI HOLELA YA AI KATIKA UTUMISHI WA UMMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 3, 2026

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI HOLELA YA AI KATIKA UTUMISHI WA UMMA


Na Okuly Julius, OKULY BLOG DODOMA


SERIKALI imewaelekeza waajiri wote nchini kuwapatia watumishi wa umma mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya Akili Unde (AI), usalama wa taarifa za Serikali na kuharakisha utatuzi wa malalamiko yanayohusu vyeo na stahili zao, huku ikionya kuwa wasimamizi watakaobainika kukwamisha haki za watumishi watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Maelekezo hayo yametolewa leo Juni 3, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, wakati akifunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo vya Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Wizara, Taasisi za Umma, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Qwaray amesema Serikali imebaini kuwepo kwa changamoto za ukiukwaji wa maadili ya utumishi, matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia pamoja na uzembe wa baadhi ya wasimamizi wa watumishi ambao umechangia kuchelewesha maendeleo ya kiutumishi kwa wafanyakazi wengi.

Amesema waajiri wote wanapaswa kuhakikisha watumishi wanatumia barua pepe rasmi za Serikali katika mawasiliano ya kikazi ili kulinda usalama wa taarifa za Serikali na kuzuia matumizi mabaya ya mifumo ya kidijitali.

“Watumishi wote wanapaswa kupewa mafunzo kuhusu usalama wa taarifa za Serikali na matumizi sahihi ya Akili Unde. Hatutavumilia matumizi ya teknolojia yanayokiuka maadili ya utumishi wa umma,” amesema Qwaray.

Aidha, ameonya kuwa watumishi watakaobainika kutumia vibaya Akili Unde au mifumo rasmi ya mawasiliano ya Serikali watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Katika hatua nyingine, Qwaray amesema Serikali imebaini kuwa baadhi ya wasimamizi walishindwa kufanya tathmini za utendaji kazi kwa mwaka 2024/2025, jambo lililosababisha baadhi ya watumishi kukosa haki zao za kupandishwa vyeo na kupata maendeleo ya kiutumishi kwa wakati.

Kutokana na hali hiyo, amemuelekeza Katibu Mkuu (Utumishi) kwa kushirikiana na waajiri wote kuwabaini wasimamizi hao na kuwachukulia hatua stahiki, ikiwemo kuwaondoa katika nafasi za uongozi pale itakapobainika walishindwa kutekeleza majukumu yao bila sababu za msingi.

Amesema Serikali pia itatafuta utaratibu wa kuwapa unafuu watumishi walioathiriwa na uzembe wa wasimamizi wao ili wasikose haki zao za kupandishwa vyeo na kunufaika na maendeleo ya kiutumishi.

Sambamba na hilo, Naibu Waziri huyo amezitaka Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika taasisi zote za umma kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utumishi ili kupunguza malalamiko ya watumishi yanayohusu kuchelewa kupandishwa vyeo, kutolipwa stahili mbalimbali, na ucheleweshaji wa gharama za uhamisho pamoja na nauli za likizo.

Amesema katika ziara zake amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa watumishi wa umma kuhusu haki zao za msingi za kiutumishi, hali ambayo imekuwa ikichangiwa na kutotekelezwa ipasavyo kwa taratibu zilizowekwa.

Qwaray amewataka wasimamizi wa Utawala na Rasilimaliwatu kuwa washauri wa karibu kwa viongozi na watumishi ili kuhakikisha haki za watumishi zinalindwa, uwajibikaji unaimarika na huduma kwa wananchi zinaendelea kuboreshwa. 

No comments:

Post a Comment