WIZARA YA FEDHA YAAINISHA VIPAUMBELE 8 BAJETI YA 2026 /2027 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 2, 2026

WIZARA YA FEDHA YAAINISHA VIPAUMBELE 8 BAJETI YA 2026 /2027


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA 


WIZARA ya Fedha imeweka mkazo katika kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kupitia mifumo ya kidijitali, kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kudumisha utulivu wa uchumi katika mwaka wa fedha 2026/27.

Hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za Serikali, kuvutia uwekezaji na kuendelea kukuza uchumi jumuishi unaowanufaisha wananchi.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Fedha alisema Serikali itaendelea kutumia teknolojia katika kuboresha ukusanyaji wa mapato, ikiwamo kukamilisha Mfumo wa Pamoja wa Kutoa Ankara za Malipo ya Serikali (Universal Billing System).

Alisema mfumo huo unatarajiwa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa ada, tozo na mapato mengine yasiyo ya kodi sambamba na kurahisisha huduma kwa wananchi na sekta binafsi.

Waziri huyo alisema Serikali pia itaendelea kuboresha na kufungamanisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na usalama wa taarifa za kifedha.

Mbali na hilo, alisema jitihada zaidi zitaelekezwa katika kuimarisha ulinzi wa mifumo ya kifedha dhidi ya mashambulizi ya kimtandao yanayoweza kuathiri utoaji wa huduma.

Katika eneo la uchumi jumla, Wizara imepanga kuendelea kusimamia sera za fedha na bajeti ili kudumisha ukuaji wa uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei na kuhakikisha deni la Serikali linaendelea kuwa himilivu.

Pia, Serikali imepanga kuimarisha usimamizi wa mali za umma kwa kukamilisha Sera ya Usimamizi wa Mali za Umma na kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usajili na ufuatiliaji wa mali hizo.

Kwa upande wa uwekezaji, Serikali itaendelea kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) kwa lengo la kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii.

Waziri huyo alisema maboresho yatafanyika pia katika mfumo wa ununuzi wa umma na ugavi ili kuongeza ufanisi, uwazi na ushiriki wa kampuni za ndani pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Aidha, Wizara imepanga kuimarisha maendeleo ya sekta ya fedha kwa kuongeza elimu ya fedha kwa wananchi, kuboresha huduma ndogo za fedha na kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara na wananchi.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha mifumo ya ukaguzi wa ndani, kudhibiti fedha haramu, kuboresha mfumo wa takwimu za taifa, kuendeleza tafiti za kisera na ubunifu pamoja na kuboresha huduma za mafao ya wastaafu na pensheni.

Waziri huyo alisema utekelezaji wa vipaumbele hivyo utaimarisha ushindani wa uchumi wa Tanzania, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea maendeleo endelevu ya taifa.

No comments:

Post a Comment