DKT. LEKASHINGO AHIMIZA UTAFITI ZAIDI KUBAINI MAENEO MAPYA YENYE MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, July 6, 2026

DKT. LEKASHINGO AHIMIZA UTAFITI ZAIDI KUBAINI MAENEO MAPYA YENYE MADINI


📍Dar es Salaam


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt.Janet Lekashingo, ameipongeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kazi kubwa inayoifanya katika kufanya tafiti za madini nchini, huku akiihimiza kuendelea kuongeza juhudi za utafiti ili kubaini maeneo mapya yenye rasilimali madini kwa ajili ya kuongeza tija katika sekta hiyo.

Dkt. Lekashingo amesema hayo alipotembelea banda la GST katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Akiwa katika banda hilo, amepata fursa ya kupokea taarifa kuhusu majukumu ya taasisi, huduma mbalimbali zinazotolewa pamoja na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa tafiti za madini nchini.

Ameeleza kuridhishwa na mafanikio yaliyopatikana hadi sasa katika shughuli za utafiti wa madini, huku akisisitiza umuhimu wa GST kuendelea kutumia teknolojia za kisasa, ubunifu na utaalamu wa watafiti wake kubaini maeneo mapya yenye rasilimali madini ambayo yataongeza fursa za uwekezaji na kuchochea ukuaji wa sekta ya madini nchini.

Aidha, amesema GST ni taasisi muhimu na nguzo ya Wizara ya Madini kutokana na jukumu lake la kufanya tafiti za kijiolojia na madini, ambazo zimeendelea kuchangia ukuaji wa sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa kupitia shughuli za utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Vilevile, ameihimiza taasisi hiyo kuendelea kuwafikia wachimbaji wadogo kwa kuwapatia huduma za kitaalamu, ushauri na elimu ya mbinu bora za utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini, akibainisha kuwa kundi hilo lina mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji wa madini, ajira na mapato ya Serikali.

GST itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kufanya tafiti za kijiolojia na madini, kutoa huduma za maabara na ushauri wa kitaalamu pamoja na kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta ya madini kwa maendeleo ya Taifa.

No comments:

Post a Comment