Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Frank Nkinda, ametoa onyo kwa wawekezaji na watu wenye uwezo wa kifedha wanaotumia nguvu zao kukiuka sheria za ardhi na kuwaonea wananchi, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita haitamvumilia mtu yeyote anayevunja sheria au kupora haki za wanyonge.
Kauli hiyo ameitoa baada ya serikali kusimamia ubomoaji wa ukuta uliodaiwa kujengwa na kuziba barabara ya wananchi katika Mtaa wa Kitwana, Kata ya Busoka, Manispaa ya Kahama, hatua iliyolenga kurejesha haki ya matumizi ya eneo hilo na kumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi na mmiliki wa shule ya awali na msingi ya Princess Mary ambaye pia ni mtumishi katika halmshauri ya Bariadi Steven Nyeriga.
Akizungumza na wananchi katika eneo hilo, Nkinda amesema moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Kahama ni migogoro ya ardhi inayosababishwa na baadhi ya watu wenye fedha wanaodaiwa kumega maeneo yasiyo yao na kuanzisha ujenzi bila kufuata taratibu za kisheria.
Amesema vitendo hivyo vimekuwa vikizalisha migogoro mikubwa kati ya wananchi na wawekezaji, huku wananchi wengi wakigundua sehemu ya maeneo yao imeingizwa kwenye hati za watu wengine kutokana na kutofahamu taratibu za umiliki wa ardhi.
"Baadhi ya wenye fedha wanatengeneza mazingira ya kumega maeneo ambayo si yao na kujenga wanavyotaka Hali hiyo imekuwa chanzo cha migogoro mikubwa kati ya wananchi na wawekezaji hivyo Serikali haitamruhusu mtu kutumia fedha au cheo chake kuwaonea wanyonge," amesema Nkinda.
Ameeleza kuwa eneo husika lina wananchi walionunua viwanja kihalali kutoka kwa wamiliki wa asili, baadhi yao wakiwa tayari wamejenga makazi yao, huku wengine wakishindwa kuendeleza maeneo yao kutokana na vitisho na ubabe uliodaiwa kufanywa na mwekezaji wa shule hiyo ya watoto.
Aidha, amewataka wawekezaji wote kufuata sheria na taratibu za ujenzi kwa kupata vibali kutoka halmashauri kabla ya kujenga nyumba au ukuta, akisisitiza kuwa hatua hiyo husaidia kuthibitisha mipaka halali ya maeneo na kuzuia migogoro isiyo ya lazima.
"Kahama tunawakaribisha wawekezaji, lakini mnapokuja lazima mheshimu sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nendeni halmashauri mpate vibali na mpimwe mipaka ili kuepusha migogoro inayowaumiza wananchi," amesema.
Nkinda pia amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na serikali za mitaa na kuiamini Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema itaendelea kusimama upande wa wananchi na kulinda haki zao bila upendeleo.
Akizungumzia hatua hiyo, Mjumbe wa Mtaa wa Kitwana, Maila, amesema mgogoro huo ulijaribiwa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo kwa muda mrefu bila mafanikio kutokana na kile alichodai kuwa ni ukaidi wa mhusika, hali iliyoilazimu serikali kuchukua hatua za utekelezaji.
"Kwa sisi kama serikali ya mtaa hili limekuwa changamoto Tulijaribu kuzungumza naye lakini ukaidi ukaendelea. Tukaona sasa kama wananchi wataachwa hivi tutasumbuka zaidi, ndiyo maana tumeshukuru serikali kuingilia kati na kuhakikisha mgogoro huu unaisha," amesema Maila.
Kwa upande wake, mkazi wa eneo hilo Joyce Paskari amesema wananchi walikuwa wakiishi kwa hofu kutokana na kile alichodai kuwa ni vitendo vya kunyanyaswa na kulazimishwa kuondoka kwenye maeneo yao bila kupenda.
"Tunashukuru sana serikali kwa kutusaidia, Tulikuwa tunanyanyaswa sana, Kuna baadhi yetu tuliokuwa tumejenga maeneo haya, mmiliki wa shule alitutaka tuhame na tuende anakotaka yeye, na ukikataa unaondolewa bila hata kulipwa fidia. Hatimaye haki imeonekana," amesema Joyce.
Naye Abduli Mugendi Kirauka amesema hatua ya serikali imewarejeshea matumaini wananchi wengi ambao walikuwa hawana uwezo wa kupaza sauti zao, akieleza kuwa mgogoro huo ulimgharimu muda mwingi wa kutafuta haki badala ya kujishughulisha na shughuli za kujipatia kipato.
"Tumeteseka sana kama wananchi, Tunashukuru serikali kwa kutuona na kutusaidia sisi wanyonge, Mgogoro huu umenichukulia muda mwingi, badala ya kutafuta chakula cha familia yangu nilikuwa nalazimika kufuatilia suala hili mara kwa mara," amesema.











No comments:
Post a Comment